Zahara Michuzi, mmoja wa watumishi wa umma waliopitia majukumu makubwa serikalini kwa miaka kadhaa, amejiunga rasmi katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Viti Maalum kupitia Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Tabora.
Katika tukio lililosubiriwa kwa bashasha na matumaini makubwa, Zahara alipokea rasmi fomu ya kugombea kutoka kwa Katibu wa UWT wa Mkoa, Bi. Rhoda Sanga. Tukio hilo limezua msisimko miongoni mwa wanachama wa UWT, huku wengi wakimtaja Zahara kama mwanamke shupavu na mchapakazi mwenye historia isiyo na doa katika utumishi wa umma.
Zahara, ambaye amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji (DED) katika Halmashauri tatu tofauti — Meatu (Simiyu), Ifakara (Morogoro), na Geita (Geita Mjini) — anajivunia rekodi ya uongozi ulioleta mabadiliko halisi katika maeneo aliyohudumu. Kabla ya kupandishwa cheo kuwa DED, aliwahi pia kuwa Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) katika Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, nafasi aliyoitumikia kwa weledi na kujenga imani kwa viongozi na wananchi.
Kwa kuingia kwake kwenye siasa, hasa katika nafasi ya uwakilishi wa wanawake kupitia UWT, Zahara analeta pamoja uzoefu wa kiutawala, usimamizi wa miradi ya maendeleo, na uelewa wa changamoto halisi zinazowakabili wanawake na jamii kwa ujumla katika mkoa wa Tabora na Tanzania nzima.
Wadadisi wa siasa wanaona uamuzi wa Zahara kama hatua ya kuhamasisha wanawake waliobobea katika sekta ya umma kushiriki moja kwa moja katika uundaji wa sera, hasa zile zinazolenga ustawi wa wanawake, vijana, na makundi maalum.