Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Rachel Kasanda kushoto,akipokea msaada wa mbao 5,000 zenye thamani ya Sh.milioni 37 kutoka kwa Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni katika Wilaya hiyo(Picha na Muhidin Amri)
Na Mwandishi Wetu,Masasi
WAKALA wa huduma za misitu Tanzania(TFS)Kanda ya kusini imetoa msaada wa mbao 5,000 zenye thamani ya Sh.milioni 37,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu Wilayani Masasi.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya Kamishina Mkuu wa TFS Profesa Dos Santos Silayo kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kasanda,Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwa amesema,wametoa mbao hizo kwa lengo la kusaidia ujenzi wa madarasa,mabweni na utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi na sekondari zilizopo katika Wilaya ya Masasi.
“Msaada huu ni sehemu ya dhamira ya TFS ya kuhakikisha kuwa rasilimali za Taifa hasa misitu na nyuki zinasimamiwa kwa njia endelevu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”alisema Mpokigwa.
Aidha alisema,msaada huo ni kuonesha shukrani kwa wananchi kwa kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na TFS katika jukumu kubwa la kulinda,kuhifadhi na kuendeleza mazingira ya Wilaya ya Masasi.
Mpokigwa alisema,Wakala wa Huduma za misitu Tanzania umeendelea kutekeleza majukumu yake kwa bidii,uadilifu na weledi mkubwa katika kusimamia,kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu na nyuki hapa nchini.
Amewashukuru wananchi wa Wilaya ya Masasi kwa kuwa sehemu ya mafanikio hayo kupitia ushirika katika shughuli za uhifadhi,kupanda miti kwa wingi na kushirikiana na TFS katika masuala mbalimbali ya kijamii yanayolenga maendeleo endelevu.
Alisema,ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa tunatunza rasilimali za misitu kwa manufaa ya watu wote huku akiwahimiza wananchi hasa walimu,wanafunzi,viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuendeleza utamaduni wa kupanda miti ya kivuli na matunda katika maeneo ya shule,zahanati na taasisi kwani itasaidia kuimarisha mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.
Mkuu wa kitengo cha uelimishaji wa TFS Kanda ya Kusini Anderson Besisila,amewataka wananchi kuendelea kutunza rasilimali za misitu kwa kutokata miti ovyo iliyohifadhiwa na kuchoma mkaa kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Alisema,TFS imeanza kampeni ya kuhamasisha jamii kuhusu matumizi ya nishati safi na salama na tayari katika Wilaya ya Masasi kuna kiwanda kikubwa cha kuzalisha mkaa mbadala kwa matumizi mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi Rachel Kasanda,ameipongeza TFS kwa kazi nzuri inayofanya katika kusimamia na kutunza rasilimali za misitu na kurudisha uoto wa asili katika maeneo yaliyoathirika na shughuli za kibinadamu.
Alisema,mbao hizo zitafanya kazi iliyokusudiwa ya kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa,mabweni na madawati ambayo yanahitajika kwenye baadhi ya shule ili watoto wapate sehemu nzuri ya kujifunzia na walimu kufundishia.
Amewaagiza Askari wa Uhifadhi wa misitu wa TFS, kuendelea kufanya doria za mara kwa mara kwenye maeneo mbalimbali ili kudhibiti uharibifu unaotokana na ukataji miti ovyo na kuhamasisha wananchi na taasisi binafsi na umma kupanda miti kwenye maeneo yao.
Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Matenkini Alokwin Chitanda alisema,mbao hizo ni msaada mkubwa kwa shule za msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Mji Masasi kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Alisema,kutokana na umuhimu wa uhifadhi wa miti wamejipnga kukomesha vitendo vyote vya uharibifu wa mazingira kwa watu wanaojihusisha na biashara ya mbao na kuchoma mkaa.

Sehemu ya shehena ya mbao zilizotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya elimu Wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara(Picha na Muhidin Amri)

Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwe akitoa taarifa ya wakala huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Rachel Kasanda kabla ya kukabidhi msaada wa mbao 5,000 zenye thamani ya Sh.ml 37(Picha na Muhidin Amri)

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Rachel Kassanda akigua shehena ya mbao zilizotolewa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya kusini,kulia kwake ni Kamanda wa TFS Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwa(Picha na Muhidin Amri)

Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara Rachel Kasanda kushoto,akipokea msaada wa mbao 5,000 zenye thamani ya Sh.milioni 37 kutoka kwa Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)Kanda ya Kusini Manyise Mpokigwa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na mabweni katika Wilaya hiyo(Picha na Muhidin Amri)