Picha ya wanawake wa kiislam wakiwa tayari kwa ajili ya kumsalimia mgeni rasmi katika kongamano la kumpongeza rais
Na. Mwandishi wetu, Katavi.
Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam (T) mkoa wa Katavi imefanya kongamano la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uongozi bora kwa kipindi cha miaka minne.
Kongamano hilo limefanyika katika ukumbi wa Mpanda Social Hall na kujumuisha wanawake wa dini ya Kiislamu pamoja na makundi ya watu mbalimbali ambao si Waislamu.
Katika kongamano hilo Watanzania wametakiwa kuwa wazalendo.
Shehe Mkuu wa mkoa wa Katavi Sheikh Nassor Kakulukulu akitoa mada katika kongamano hilo amesema uongozi si suala la kuchezea.
“Kiongozi ni mtu mwenye wafuasi. Tunampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu katika nchi yetu kwa sababu kwa yale aliyoyafanya tumeyaona na tumeyakubali” alisema.
Shehe Kakulukulu aliongeza kuwa vijiji 172 vya mkoa wa Katavi vyote kwa sasa vina umeme tofauti na siku za nyuma ambapo ametoa mfano kuwa ilikuwa lazima ufunge dumu la mafuta ya taa kwenye baiskeli kwa ajili ya chemli yako au koroboi!
Aidha shehe huyo wa mkoa wa Katavi ameeleza kuwa hata maendeleo ya dini hayawezi kufikiwa kama maendeleo mengine hayajafikiwa.
Pia amewataka Waislamu wasikubali kupotoshwa na watu wasiopenda amani.
Kwa upande wake mwenyekiti wa JUWAKITA mkoa wa Katavi bi. Tatu Abdallah Nkana amewataka kinamama kuendeleza ushirikiano walionao katika kila jambo.
“Ndugu zangu ushirikiano huu usiwe na mipaka tuuendeleze na taasisi mbalimbali za kiserikali na za binafsi, kwani bila ushirikiano hakunajambo litakalofanikiwa” alisema Tatu.
Mkuu wa wilaya ya Mpanda bi. Jamillah Yusuf amesema kiasi cha shilingi bilioni 218 zilipokelewa katika wilaya hiyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza katika kongamano hilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Katavi; mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj majid Mwanga amempongeza rais kwa kipindi cha miaka minne aliyoko madarakani.
Alhaj Mwanga alisema katika kipindi hicho Tanzania imeshuhudia mabadiliko makubwa katika ujenzi wa wa miundombinu ikiwemo madaraja, meli, barabara, umeme na elimu.
“Kwenye afya napo vituo vya kutolea huduma vimeongezeka na hata ya huduma za kuchuja na kusafisha figo hivi sasa zinapatikana hapa mkoani na hivyo kupunguza adha ya kutafuta huduma hiyo mbali katika mikoa mingine” alisema.
“Kwa wakulima, Mh. Rais alipofika hapa mwaka jana alituzindulia Ghala la mazao ambalo limesababisha bei ya mazao kwa wakulima wa mahindi na mpunga kuwa nzuri” aliongeza.
Aidha amewaasa wanakatavi kulinda amani iliyopo na kutoa taarifa za wageni wanaoingia bila kufuata taratibu za nchi.
Halikadhalika amewataka wananchi wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu na kuhakikisha wanachagua viongozi makini na waadilifu katika maeneo yao.
“Mwisho, rai yangu kwenu ni kuhakikisha kila familia inahifadhi chakula” alihitimisha Alhaj Mwanga.
Jumuiya hiyo imempa tuzo mama Samia ya kuboresha afya ya mama na mtoto.
Pia imetoa tuzo kwa mkuu wa mkoa wa Katavi kwa kuhamasisha lishe bora ili kupunguza udumavu.