Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Julai 2, 2025
Jumla ya wanawake wanne wamejitokeza kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, mkoani Pwani, akiwemo Wakili Msomi Magreth Mwihava.
Kwa upande wa wanaume, wagombea waliokwisha kuchukua fomu hadi kufikia Julai 1, 2025 wamefikia 13.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini, Isaack Kalleiya, alisema kuwa hadi kufikia tarehe hiyo jumla ya wagombea 17 wamechukua fomu za kuwania ubunge kupitia chama hicho.
Wakili Magreth Mwihava, ambaye ni mmoja wa wanawake waliotangaza nia, alisema ameamua kuchukua fomu kwa sababu anaamini katika uwezo wake kama mwanamke jasiri na mwenye maono. Hata hivyo, alieleza kuwa kwa sasa anasubiri uamuzi wa vikao vya chama.
Wagombea wengine waliokwisha kuchukua fomu ya ubunge katika jimbo hilo ni pamoja na Mussa Mansour, Godwin Ndosi, Ibrahim Mkwiru, Abubakar Allawi , Dkt. Charles Mwamwaja na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Silvestry Koka.
Wakati huo huo, katika upande wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Kibaha Mjini, jumla ya wagombea 31 wa viti maalum vya udiwani wamejitokeza hadi sasa, akiwemo Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Pwani, Tatu Kondo.
Tatu alipokea fomu yake kutoka kwa Katibu wa UWT Kibaha Mjini, Cecilia Ndalu.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu, Tatu alieleza, watu wenye ulemavu wana uwezo sawa wa kuwatumikia wananchi na kushiriki katika nafasi za maamuzi kama ilivyo kwa watu wengine.
Aliongeza kusema, atafurahia kuona kundi la watu wenye ulemavu likipata nafasi katika uongozi kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.