Na Silivia Amandius, Bukoba
Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera linawashikilia wanaume wawili kutoka mkoani Songwe kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya binadamu, tukio linalozua maswali mengi kuhusu usalama na maadili ya kijamii.
Watuhumiwa hao ni Kelvin Piason Mdolon (42), mkazi wa Mnyiha na mganga wa kienyeji pamoja na Randani Seme Mlomo (64), mkazi wa Mnyamwanga ambaye ni mtumishi wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Vwawa wilayani Mbozi, mkoa wa Songwe.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Blassius Chatanda, alieleza kuwa Kelvin Mdolon alikamatwa tarehe 17 Juni mwaka huu akiwa na viungo vya binadamu. Alipohojiwa, alidai kuwa alihitaji kuvitumia kwa matumizi yake binafsi.
Katika mahojiano na vyombo vya dola, Kelvin alimtaja Randani Mlomo kuwa ndiye aliyempatia viungo hivyo vya binadamu kutoka chumba cha kuhifadhia maiti. Hii ilipelekea jeshi la polisi kumkamata na kuendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini undani wa tukio hilo na mtandao wake iwapo upo.
Kamanda Chatanda ametoa wito kwa wananchi wa Kagera kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa pale wanaposhuhudia matukio yasiyo ya kawaida katika jamii.
Aidha, ametoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na shughuli za uganga wa jadi bila kuwa na vibali halali, akisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kudhibiti vitendo vinavyohatarisha maisha ya watu na kukiuka sheria za nchi.
Upelelezi wa tukio hilo unaendelea.