Dar es Salaam, Tanzania – Chama cha Wastaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BOTRA) kimefanya mkutano wake mkuu wa mwaka ukiwa na lengo la kujadili maendeleo, ustawi na mustakabali wa wanachama wake pamoja na maisha ya wastaafu kwa ujumla nchini.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa BOTRA, Bi. Grace Rubambey, alisisitiza kuwa kustaafu siyo mwisho wa maisha ya kitaaluma, bali ni mwanzo wa hatua mpya yenye fursa mbalimbali kwa wastaafu kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii.
“Kustaafu haimaanishi kuwa mtu amemaliza kutoa mchango wake kwa taifa. Maarifa na uzoefu wa wastaafu vina thamani kubwa. Kupitia BOTRA, tunawawezesha wanachama wetu kuendelea kuwa na mchango chanya na kuheshimiwa katika jamii,” alisema Bi. Rubambey.
Aliongeza kuwa kuanzishwa kwa BOTRA ni hatua muhimu ya kimkakati inayolenga kuwaleta pamoja wastaafu wa Benki Kuu ya Tanzania ili kushirikiana, kutetea maslahi yao, na kuendeleza ushirikiano wa kitaaluma na kijamii hata baada ya kustaafu.
Mkutano huo uliwakutanisha wanachama kutoka mikoa mbalimbali nchini, ambapo walijadili mambo muhimu yakiwemo mikakati ya kuboresha huduma za afya kwa wastaafu, fursa za kiuchumi, mafao ya uzeeni, na njia za kuimarisha uhusiano na taasisi za kifedha na serikali.
BOTRA imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwahamasisha wastaafu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kielimu, ikiwa ni pamoja na kushiriki midahalo ya sera zinazowahusu moja kwa moja.