Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe amesema kuwa watumishi wa WIzara ya Afya waliopo makao makuu Dodoma, watahamia rasmi kwenye jengo jipya la Wizara lililopo katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma kuanzia tarehe 20 Julai 2025.
Dkt. Shekalaghe amesema hayo leo Julai 3, 2025 alipoiongoza menejimenti ya Wizara ya Afya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo na mipango ya kuhamia katika ofisi hizo.
Ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 96 hadi sasa huku ujenzi wa jengo la Wizara ya Afya hadi kukamilika kwake utagharimu zaidi ya Shilingi Bilioni 26.6.
Jengo hilo lina mita za mraba 14,355 likijumuisha sakafu kumi (10) mbili zikiwa ni sakafu za ardhini (basement), jengo litakuwa na ofisi zaidi ya 188 pamoja na kumbi za mikutano 13.