Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Mkuu wa Mkoa Katavi Mwanamvua Hoza Mrindoko ameeleza kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2025 Mkoa wa Katavi ulikuwa umeunganishwa na Umeme wa Gridi ya Taifa na kuwashwa katika Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Nsimbo na Wilaya ya Tanganyika ambapo gharama za mradi huu zilikuwa ni bilioni 116 kutokea Mkoa wa Tabora 132 KV.
RC Mrindoko ameyaeleza hayo leo Jijini Dodoma Julai 3,2025 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akielezea mafanikio ya Mkoa huo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.
Ambapo amesema hapo awali kabla ya kuunganishwa katika Gridi ya Taifa Mkoa huo na Wilaya zake ulikuwa ukipata umeme unaofuliwa katika vituo viwili vilivyopo Mpanda mjini ambavyo vilikuwa vinatumia mafuta mazito ya Dizeli huku Halmashauri ya Mpimbwe ilikuwa ikipokea Umeme kutoka Sumbawanga ambayo ni gridi ya Taifa ya Zambia.
“Ndugu Zangu, Mkoa wa Katavi pamoja na Wilaya zake ulikuwa unapata Umeme unaofuliwa katika vituo viwili (2) vilivyopo Mpanda Mjini (MW 7.5) na Mlele (MW 1.44) ambavyo vinatumia mafuta mazito ya dizeli ambapo Halmashauri ya Mpimbwe ilikuwa inapokea Umeme kutokea Sumbawanga ambao ni wa Gridi ya Taifa ya Zambia eneo la Mbala”.
“Hadi kufikia mwezi Juni, 2025 Mkoa wa katavi umeunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa na umewashwa katika Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Nsimbo na Wilaya ya Tanganyika. Gharama za Mradi huu ni shilingi billion 116 kutokea Mkoa wa Tabora 132KV. Mradi umehusisha ujenzi wa njia kubwa ya Umeme ya msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi umbali wa kilomita 383 na kujenga vituo viwiwli vya kupoozea Umeme katika eneo la Inyonga kituo chenye ukubwa wa 12MW na eneo la Mpanda kituo chenye ukubwa wa 28MW”.
Aidha amesema kuwa Katika kipindi cha uongozi wa Rais wa awamu ya Sita, Mkoa umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 196.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Umeme ikiwemo Upanuzi wa mtandao wa Umeme kwa Wilaya ya Mpanda, Tanganyika na Mlele, Kuongeza nguvu ya Umeme kwa Wilaya ya Mpanda, Tanganyika na Mlele, kupeleka Umeme kwenye Vijiji kwa ufadhili wa REA awamu ya kwanza katika Vijiji vyote 172 vya Mkoa na vina Umeme ambapo pia hadi kufikia Juni, 2025 Vitongoji 504 kati ya Vitongoji 912 vya Mkoa wa katavi vimeunganishiwa umeme na Vitongoji 408 vilivyo baki vitaunganishwa katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2025/2026.
Ambapo upelekaji wa huduma hizi umeongeza idadi ya wateja wanao tumia Umeme kutoka wateja 23,312 mwaka 2020/21 hadi wateja 42,567 Juni, 2025 na kuleta chachu ya ongezeko la mapato kutoka shilingi 494,496,385.22 hadi shilingi 1,031,280,772.87 kwa mwezi.
Pia ameongeza kuwa kwa upande wa Sekta ya Maji Mkoa umeendelea kutekeleza miradi MITANO yenye thamani ya Shilingi bilioni 32,163,080,399.89 ambayo ikikamilika itaongeza upatikanaji wa Maji kwa zaidi ya asilimia 100 kwani Mkoa unaendelea kutekeleza mradi wa usamabazaji Maji kutoka Bwawa la Milala unaotekelezwa chini ya mpango wa ujenzi wa mradi wa Maji wa Miji 28 na Mradi huu unatarajiwa kuzalisha Maji lita 12,000,000 kwa siku na kunufaisha wakazi wote wa Manispaa ya Mpanda.
Mkoa huu wa Katavi ni Mkoa ulioanzishwa Mwaka 2012 ukigawanywa kutoka katika Mkoa wa Rukwa.