Wananchi wakiwa katika Banda la Kampuni ya Jovisa Cooling lililopo ndani ya Banda la Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba wakipewa elimu ya fursa mbalimbali za kiuchumi.
NA NOEL RUKANUGU, DAR ES SALAAM
Wananchi wametakiwa kutembelea Banda la Kampuni ya Jovisa Cooling lililopo ndani ya Banda la Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, ili kujifunza fursa mbalimbali ikiwemo namna ya kujiajiri kupitia fani za ufundi zinazotolewa na VETA.
Kampuni ya Jovisa Cooling ni miongoni mwa wabobezi nchini Tanzania katika ufungaji na utengenezaji wa mashine za viyoyozi (AC), ambapo imetekeleza miradi mingi katika taasisi za umma na sekta binafsi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Jovisa Cooling, Bw. Joseph Sangawe, alisema kuwa baada ya kuhitimu shahada yake kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alijiunga na VETA kwa ajili ya kupata mafunzo ya vitendo katika fani ya ufundi wa viyoyozi.
“Baada ya kumaliza mafunzo ya kufunga na kutengeneza mashine za AC, nilianzisha kampuni hii, ambayo imekuwa na mafanikio makubwa na pia imeniwezesha kuajiri vijana wengi,” alisema Bw. Sangawe.
Aliongeza kuwa amekuwa akikutana na vijana waliohitimu elimu ya juu na kuwashauri kujifunza pia fani za ufundi, ili kuwawezesha kujiajiri na kuongeza ujuzi wao.
“Vijana wengi nimekuwa nikiwahamasisha kusoma fani mbalimbali hata baada ya kuhitimu vyuo vikuu. Nitaendelea kuwafundisha na kuwawezesha kufikia malengo yao,” alisisitiza.
Aidha, alieleza kuwa kusoma fani za ufundi ni muhimu kwa ajili ya kuongeza ajira kwa vijana na kujiongezea thamani katika soko la ajira.
“Tuwaunge mkono viongozi wetu kwa sababu wana malengo mazuri ya kutupeleka mbele kimaendeleo, hususan katika kukuza uchumi,” alisema Bw. Sangawe.
Akihitimisha, Bw. Sangawe alisifu mchango wa VETA katika maendeleo ya vijana, akisema ni taasisi yenye mchango mkubwa katika kuwawezesha vijana wengi kufanikisha ndoto zao.