Mikumi, Tanzania – Julai 5, 2025
Wakuu wa Divisheni na Vitengo kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wametembelea Mbuga ya Wanyama ya Mikumi katika ziara maalum yenye lengo la kuhamasisha utalii wa ndani na kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza sekta ya utalii nchini.
Ziara hii imeongozwa na Afisa Utumishi wa Manispaa hiyo, Bw. Mrisho Mlela, ambaye amesema kuwa kama menejimenti wameamua kuwa sehemu ya juhudi za serikali kwa njia ya vitendo, kwa kuwahamasisha watumishi kushiriki katika utalii wa ndani.
“Tumeona ni muhimu sisi kama viongozi na watumishi wa umma kuonesha mfano kwa kutembelea vivutio vya ndani ya nchi. Hii ni njia mojawapo ya kuunga mkono kampeni ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha utalii wa ndani, ambayo inalenga kuongeza mapato ya ndani kupitia sekta hii muhimu,” alisema Bw. Mlela.
Ziara hiyo pia inawapa nafasi washiriki kujifunza zaidi kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia utalii wa ndani.
Mbuga ya Mikumi ni mojawapo ya vivutio maarufu vya utalii nchini, inayopatikana katika mikoa ya Morogoro na Pwani, na ina aina mbalimbali za wanyama kama tembo, simba, twiga, pundamilia na nyati na wengine wengi.