-Waomba ushirikiano katika suala la Nishati Safi ya Kupikia
Wanufaika wa Mradi wa ARDHI (Accelerating Reforestation for the Development of Households) wa Mkoa wa Tanga wametembelea Banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam Julai 6, 2025 kwa lengo la kujifunza mbinu bora za kuhifadhi mazingira na kujiongezea kipato kupitia miradi ya nishati safi ya kupikia.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika hao wa mradi unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Shirika lisilo la Kiserikali la World Vision Tanzania, Audiphonce Jonas alisema mradi huo umejikita katika suala la uhifadhi wa mazingira.
“Tumefika hapa katika banda la REA kwa ajili ya kujifunza namna ambavyo tunaweza kutumia nishati safi ya kupikia kutimiza azma yetu ya kuhifadhi mazingira sambamba na kuona ni vipi tunaweza kuitumia kujipatia kipato,” alisema Jonas.
Alisema mradi umeanza mwaka huu na utafika kikomo mwaka 2027 na unanufaisha wilaya nne za Mkoa wa Tanga ambazo ni Pangani, Kilindi, Mkinga na Handeni.
Alisema lengo la mradi ni kuwa na usimamizi endelevu wa misitu na hilo linafanyika kwa kubuni njia mbadala za matumizi ya kuni na mkaa ambazo ndio chanzo kikuu cha nishati ya kupikia kwa wakazi wa wilaya hizo.
“Lengo la mradi huu wa ARDHI ni sawa na kinachotekelezwa na REA; itakuwa vyema REA ikatazama namna ya bora ya kushirikiana nasi katika hili jukumu la uhifadhi wa misitu,” alisema.
Alisema kwa sasa mradi unashirikiana kwa karibu na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na ni wakati sahihi pia kushirikiana na REA kupitia miradi yake ya Nishati Safi ya Kupikia.
“Tunaipongeza REA kwani tumeshuhudia hatua kubwa imepigwa; tumejionea bidhaa mbalimbali za nishati safi ya kupikia zilizotengenezwa kwa teknolojia iliyoboreshwa,” alisema.
Alisema malighafi za utengenezaji wa bidhaa mbakimbali za nishati safi ya kupikia ikiwemo mkaa mbadala zinapatikana kwa wingi katika maeneo yao hivyo itakuwa jambo rahisi kuanzisha miradi ya nishati safi ya kupikia.