Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji uliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani Tlkatika ukumbi wa Hoteli ya Polana Serena, jijini Maputo Tarehe 07 Julai 2025,
Tukio hilo lilihudhuriwa na wadau kutoa makundi mbalimbali wakiwemo; Wawakilishi wa Serikali ya Msumbiji; baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini Msumbiji; Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa; Wanazuoni wa lugha na Tamaduni za Kiafrika; Viongozi Wahariri wa vyombo vya Habari na Diaspora wa Tanzania nchini Msumbiji.
Miongoni mwa Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo ni Mhe. Philip Mundia Githiora, Balozi wa kenya nchini Msumbiji ambapo alipata fursa ya kuzungumza na kueleza mafanikio ya Lugha ya Kiswahili. Katika maelezo yake alifafanua kuwa lugha hii ni urithi na alama ya umoja kwa nchi za Afrika Mashariki na Bara zima kwa ujumla. Hivyo, alilisisitiza kuwa ni vema kutumia lugha hii kama nyenzo ya kudumisha uhusiano na ukaribu wa nchi za Afrika.
Hafla hiyo iliambatana na burudani mbalimbali mathalan, ngoma ya asili ya Kimakonde, Makala za maonesho ya bidhaa na rasilimali mbalimbali za Taifa na kuonesha hatua za Maendeleo zilizofikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta mbalimbali.
Aidha, Hafla hiyo ilihitimishwa na hotuba ya Mhe. CP. Hamad Khamis Hamad, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji ambapo alihamasisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili katika ukanda wa kusini mwa Afrika hususan katika nchi zilizo katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Vilevile, alisisitiza Kukuza utamaduni wa Kiswahili kama chombo cha kuunganisha jamii kutoka Mataifa mbalimbali, kuendeleza Elimu na Diplomasia, pamoja na kuonesha mchango wa Tanzania katika kuendeleza Kiswahili. Kadhalika, alieleza kwa kina chimbuko la Lugha ya Kiswahili na mafanikio yake yakiwemo ongezeko la wazungumzaji duniani kote.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania – Maputo