Wizara ya Katiba na Sheria imeibuka mshindi wa kwanza kati ya wizara zote zilizoshiriki katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba, yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Barabara ya Kilwa.
Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye maonesho hayo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, aliwataka wananchi kutembelea banda la wizara hiyo ili kupata elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria.
Alieleza kuwa wananchi wameonyesha mwitikio mkubwa na kuridhika na huduma zinazotolewa, hasa msaada wa kisheria na elimu kuhusu Katiba.
“Wananchi wengi wamefika kupata elimu na msaada wa kisheria. Nawapongeza wataalamu wetu pamoja na mawakili waliopo hapa kwa kujitolea kwao kutoa huduma muhimu kwa jamii,” alisema Sagini.
Akiwa kwenye ziara hiyo, Naibu Waziri pia alitembelea Banda la Mahakama na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), ambapo alishuhudia idadi kubwa ya wananchi wakihudumiwa hususan katika kupata vyeti vya kuzaliwa.
Alikumbusha kuwa huduma kama hizi zinapatikana hadi ngazi ya wilaya hivyo si lazima kusubiri maonesho.
Sagini aliishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vya maonesho na kuwezesha taasisi mbalimbali kufikisha huduma karibu zaidi na wananchi.
Kwa upande mwingine, aliangazia umuhimu wa kampeni ya msaada wa kisheria, akisema serikali imeweka kipaumbele kueneza huduma hiyo hadi kwenye halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sheria.
Pia, alisisitiza umuhimu wa elimu ya sheria katika masuala kama ardhi na ndoa, ambapo migogoro mingi hutokana na ukosefu wa uelewa wa kisheria.
Alitoa wito kwa maafisa wa serikali za mitaa na wataalamu wa msaada wa kisheria kuendelea kutoa elimu hiyo kwa jamii.