Naibu Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis amesema Maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam ni fursa kwa Wazanzibari kutangaza utamaduni wao, bidhaa za asili, Utalii, fursa za biashara zao pamoja na uwekezaji.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleao ya viwanda Dkt. Said Seif Mzee alimkaribisha Mgeni rasmi katika Siku ya Zanzibar”Zanzibar Day” iliyogusia mila, Silka na Utamaduni wa Zanzibar, fursa na mwelekeo wa uwekezaji endelevu na kufungua milango ya biashara.
Aidha siku ya Zanzibar”Zanzibar Day” iliambatana na majadiliano yaliyoangazia fursa mbalimbali zinazopatikana Zanzibar ikiwemo Utalii, Uchumi wa Buluu, Uwekezaji na Biashara.
Katika Siku hiyo maalumu ushiriki wa Chemba ya biashara, Viwanda na kilimo Tanzania(TCCIA) uliwakilishwa na Mkurugenzi mtendaji Bw. Oscar Kissanga ikiwa ni Ishara ya taasisi hiyo kuunga mkono juhudi za serikali katika kutanga tamaduni na kukuza bidhaa na huduma zinazotoka Zanzibar na Tanzania bara kwa ujumla, pamoja na kuimarisha matumizi ya bidhaa za ndani kama kichocheo cha maendeleo ya viwanda, ajira, na ushirikiano wa kibiashara kati ya pande mbili za Muungano.