-Dar es Salaam, Julai 9, 2025
Katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, Tume ya Madini imeeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana kufuatia uwekaji wa uzio kuzunguka Mgodi wa Tanzanite uliopo Mirerani, mkoani Manyara.
Akizungumza katika banda la Tume Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi -Mirerani, Bw. Adolf Robert, amesema kuwa hatua ya kujenga uzio kuzunguka mgodi huo imeleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato na kudhibiti utoroshaji wa madini.
“Kabla ya kuwekwa kwa uzio, mapato kutoka mgodi wa Mirerani yalikuwa chini ya Shilingi milioni 200 kwa mwaka. Hivi sasa, baada ya uwekaji wa uzio, mapato yameongezeka hadi zaidi ya Shilingi bilioni mbili kwa mwaka,” amesema Robert.
Kwa mujibu wa mtaalam huyo, mbali na Tanzanite ambayo ni madini adimu yanayopatikana Mirerani pekee duniani, eneo hilo pia yanapatikana madini mengine ya vito kama vile green garnet, tourmaline, rhodolite, ruby na moonstone, ambayo yanaendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameeleza kuwa eneo hilo pia lina madini ya kimkakati kama graphite (kinywe), ambayo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme na mashine za viwandani, hivyo kutoa fursa kubwa kwa wawekezaji wa teknolojia ya kisasa.
Robert amebainisha kuwa uwekaji wa uzio huo umeongeza usalama katika eneo la mgodi, kurahisisha usimamizi wa shughuli za uchimbaji, na kuwa kichocheo cha uwekezaji endelevu.
“Maonesho haya yanatoa fursa adhimu kwa wananchi na wawekezaji kujifunza kwa kina kuhusu sekta ya madini, ikiwa ni pamoja na taratibu za kupata leseni, teknolojia ya uongezaji thamani, na namna bora ya kuwekeza,” ameongeza.
Tume ya Madini imeendelea kutumia jukwaa la Sabasaba kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa madini katika kukuza uchumi wa nchi, sambamba na kueleza mikakati ya Serikali ya kuhakikisha sekta hiyo inachangia kikamilifu kwenye pato la Taifa.
Kwa ujumla, mafanikio ya uwekaji uzio katika mgodi wa Mererani ni ushahidi tosha kuwa usimamizi madhubuti wa rasilimali za taifa unaweza kuleta tija kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira.