Na Neema Mtuka Nkasi.
Rukwa :Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dr.Edwin Mhede amezindua chanjo za mifugo zinazotolewa kwa Ruzuku ya Serikali Kimkoa katika Ranchi ya Kalambo iliyopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Mkoa wa Rukwa.
Naibu Katibu Mkuu huyo amezindua Chanjo ya Ugonjwa wa Homa ya Mapafu kwa ng’ombe (Contagious Bovine Pleuropneumonia-CBPP) ambayo itatolewa kwa nusu ya bei halisi ambapo mfugaji atachangia shilingi 500 tu kwa dozi ya ng’ombe mmoja.
Utoaji wa Chanjo hiyo utaenda sambamba na utambuzi kwa njia ya heleni ambayo itatolewa bila malipo kwa kila ng’ombe atakayechanjwa.
Sambamba na hilo pia katibu mkuu Mhede amezindua Chanjo ya tatu moja kwa kuku ambayo inazuia magonjwa matatu kwa wakati mmoja ambayo ni Mdondo/Kideri,Ndui ya Kuku na Mafua ya kuku yanayoambukiza ambayo itatolewa kwa Ruzuku ya Serikali kwa asilimia 100.
Mhede amewataka wananchi wajitokeze kuleta mifugo yao kwenye vituo vya chanjo kwani chanjo hizo ni Salama na zitakinga mifugo yao dhidi ya magonjwa ambayo yanasumbua sana mifugo hapa Nchini na hivyo kuongeza uzalishaji na tija ya Ufugaji.
Ameongeza kuwa mifugo yetu itakapochanjwa itakuwa na afya bora hali itakayoongeza fursa zaidi katika masoko ya nje na kuongeza kipato cha mfugaji na Taifa kwa ujumla .
“Niwatake wafugaji tujitokeze tukachanje mifugo yetu maana “ujanja ni kuchanja mifugo” .
Aidha amewasisitiza wataalam kukamilisha zoezi la chanjo kufikia Oktoba 2025.