▫️Washindi medali za Dhahabu
▫️Tanzania yawa washindi wa pili wa jumla
▫️R&J Mazola mwamuzi bora wa mashindano
8-07-2025, Moroni – Comoros.
MABONDIA Kassim Mbundwike na Ezra Paulo wamefanikiwa kushinda mapambano yao ya fainali za President Cup nchini Comoros usiku wa kuamkia leo na kushinda medali za Dhahabu, simu janja na vikombe vya uchezaji bora.
Mapambano hayo yaliyoshuhudiwa na Rais wa Comoros Mh. Azali Assoumani katika uwanja wa michezo wa Malouzini ambapo Mbundwike alishinda kwa points 2-1 dhidi ya Soilihi Anzali kutoka Comoros katika uzani wa 75kg, huku katika uzani wa 60kg Ezra akishinda kwa points za majaji 2-1 dhidi ya Radjay Mohamed wa kutoka Comoros.
Pamoja na ushindi huo wa Mbundwike na Ezra, walipewa zawadi ya simu janja “smartphones” kutoka kampuni ya YAS ambao walikua moja ya wadhamini wa mashindano hayo.
Katika mapambano mengine, mabondia Kaimu Kaimu na Rashidi Mrema walipata medali za fedha licha ya wote kupoteza mapambano yao kwa points 2-1 dhidi ya Mohamed Ali kutoka Comoros katika uzani wa 54kg dhidi ya Kaimu na Ilzam Taoufik wa Comoros katika uzani wa 63.5 aliyecheza na Mrema.
Tanzania imemaliza kwa kushinda Kombe la nafasi ya pili ya jumla huku Mwamuzi na Jaji wa Kimataifa wa Nyota 1 Ramadhani Mazola akichaguliwa mwamuzi bora kati ya 12 wa mashindano hayo na kutunukiwa kikombe, medali na cheti kwa mafanikio yake.
“Tunaendelea kuvuna matunda ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na Shirikisho katika kuwaendeleza kimafunzo wataalamu na wasimamiaji wa mchezo wa ngumi kwa ngazi za kitaifa na kimataifa.” alinukuliwa Rais wa BFT Ndg. Lukelo Willilo.
Wakati huo, Balozi wa Tanzania nchini Comoros Mh. Said Yakubu aliwashukuru na kuwapongeza wachezaji na uongozi mzima kwa kufanya vizuri na kuliheshimisha Taifa katika mashindano hayo.
Mashindano hayo yalishirikisha mataifa 4 ambayo ni wenyeji Comoros waliomaliza wa kwanza, wakifuatiwa na Tanzania (2), Gabon (3) na Madagascar (4) huku timu ikitarajia kurejea leo kwa usafiri wa shirika la ndege la Air Tanzania.