Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi (Mb.), kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mohamoud Thabit Kombo (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Misheni ya Awali ya Uangalizi wa Uchaguzi ya SADC Jula 11, 2025 katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam. Misheni hiyo inaongozwa na Bi. Jennifer Chiringa, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri ya Uchaguzi la SADC ambae ni raia wa Zimbabwe.
Wakati wa mazungumzo ya viongozi hao, Mhe. Chumi aliwakaribisha Tanzania na kuahidi kuwa Serikali itashirikiana na Misheni hiyo ili iweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.Aliwahakikishia SEAC kwamba Tanzania iko tayari kwa uchaguzi na utafanyika katika mazingira ya amanu na usalama. Misheni hiyo ipo nchini ili kuzungumza na wadau mbalimbali wa uchaguzi na kufanya tathmini ya hatua zilizofikiwa katika kufanya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa huru na haki mwezi Oktoba, 2025.
Pamoja na masuala mengine, Misheni hiyo itakutana na wadau mbalimbali ikiwemo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), baadhi ya Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, Msajili wa Vyama vya Siasa, Baraza la Vyama vya Siasa, Taasisi za Vyombo vya Habari, na Asasi za kirai na kufanya nao mazungumzo.
Aidha, katika mazungumzo hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masula ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (MB.) na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Balozi Said Mussa walishiriki.