USHIRIKIANO wa kiuchumi kati ya Tanzania na India unaendelea kuimarika kwa kasi, huku India ikijidhihirisha kama mmoja wa wawekezaji wakubwa na wa kuaminika nchini. Takwimu kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) zinaonesha kuwa hadi sasa, jumla ya miradi 793 kutoka India imesajiliwa rasmi, ikiwa na thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.5.
Miradi hiyo imejikita zaidi katika sekta za viwanda, usafirishaji na miundombinu ya kibiashara – ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa India katika mazingira ya biashara nchini Tanzania.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), jijini Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Siku ya India, Mkurugenzi Mtendaji wa TISEZA, Gilead Teri, amewakaribisha wawekezaji kutoka India kuendelea kushirikiana na kampuni za Kitanzania ili kuzalisha bidhaa kwa ajili ya soko la ndani, Afrika, na masoko ya kimataifa kama Ulaya na Marekani, ambako bidhaa kutoka Tanzania zinaingia bila ushuru wala vikwazo.
“Kituo cha Uwekezaji kimejipanga kutoa msaada na taarifa zote muhimu kwa wawekezaji. Tunawakaribisha kutembelea banda letu la TISEZA katika maonesho haya ili wajifunze kwa undani fursa zilizopo Tanzania,” alisema Teri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Latifa Khamis, alisisitiza dhamira ya kuendeleza ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na India, hasa kupitia wadau kutoka Jimbo la Haryana, ambalo limeonyesha nia ya dhati kushirikiana katika maeneo ya teknolojia, kilimo na viwanda vidogo.
“Maonesho ya mwaka huu yamevutia zaidi ya washiriki 4,000, jambo linalothibitisha kuwa Tanzania ni kitovu cha kibiashara cha kuaminika Afrika Mashariki. TanTrade itaendelea kusaidia biashara ndogo na za kati kupitia ushauri wa chapa, matumizi ya teknolojia rahisi, na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa,” alibainisha Latifa.
Kutoka Jimbo la Haryana, Mkurugenzi wa FCD, Amna Tasneem, alitoa wito kwa wafanyabiashara wa India na Tanzania kuimarisha ushirikiano uliopo ili kufanikisha makubaliano yaliyokwisha anzishwa na kuleta maendeleo endelevu kwa pande zote mbili.
Miongoni mwa kampuni zilizoshiriki ni Shirika la Uhifadhi wa Mazao la Jimbo la Haryana (HSWC), ambalo limepata mafanikio makubwa katika ununuzi na uhifadhi wa mazao kwa kutumia teknolojia ya kisasa – kwa upotevu wa mazao usiozidi asilimia 0.2.
“Tuna mapato ya zaidi ya dola milioni 588 kwa mwaka, na tuko tayari kusaidia Tanzania kwa kujenga maghala ya kisasa, kutoa mafunzo kwa wakulima, na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno,” ilielezwa na mwakilishi wa HSWC.
Kwa upande wa teknolojia, Shirika la Maendeleo ya Elektroniki la Haryana (HATRON) lilitangaza kusaini makubaliano ya ushirikiano na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa lengo la kuanzisha vituo vya mafunzo ya TEHAMA nchini Tanzania.
“Tuna mtandao mpana wa vituo vya mafunzo ya IT nchini India, na tunataka uzoefu huo kuwanufaisha vijana wa Tanzania ili waweze kuajiriwa au kujiajiri kupitia teknolojia ya kisasa. Tuko tayari kushirikiana na serikali, vyuo na sekta binafsi nchini Tanzania ili kuharakisha maendeleo ya kidijitali,” alisema mwakilishi wa HATRON.