Na Fauzia Mussa
MAKAMU Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Mbarouk Salim Mbarouk, amewataka waratibu wa uchaguzi, wasimamizi na wasaidizi wao katika ngazi ya majimbo kuhakikisha wanawafundisha kwa weledi watendaji wa vituo vya kupigia kura ili kuimarisha ufanisi na uadilifu wa zoezi la uchaguzi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu yaliyofanyika katika Ukumbi wa Polisi Ziwani, Jaji Mbarouk alisisitiza umuhimu wa mafunzo hayo, akisema:
“Ni lazima mtoe mafunzo sahihi kwa watendaji wa vituo. Hili ni jukumu lenu. Lazima kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa haki, amani na kwa kuzingatia sheria na kanuni za Tume.”
Alisisitiza pia juu ya umuhimu wa kuhakiki vifaa vya uchaguzi mara tu vinapopokelewa na kutoa taarifa haraka kwa Tume endapo kuna upungufu wowote.
Vilevile, aliwataka wasimamizi hao kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali, ikiwemo fedha, kwa uwazi na uadilifu.
Jaji Mbarouk alikumbusha kuhusu kiapo cha kutunza siri walichokula kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo na kuwaonya dhidi ya uvujishaji wa taarifa, hasa kupitia mitandao ya kijamii kama WhatsApp.
“Ni kosa kisheria kutoa taarifa za siri za uchaguzi. Mnapaswa kupunguza matumizi ya mitandao ya kijamii ili kuepuka hata kwa bahati mbaya kutuma taarifa isiyokusudiwa,” alisema kwa msisitizo.
Aliwakumbusha pia kuhusu jukumu lao la kuhakikisha ubandikaji wa mabango ya uchaguzi unafanyika kwa mujibu wa kalenda ya Tume, ili kuepuka malalamiko kutoka kwa wagombea na wadau wa uchaguzi.
Ramadhani Abdalla Bakar, Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, alisema kuwa washiriki walifaidika kwa kiwango kikubwa na mafunzo hayo ambayo yalijumuisha nadharia na vitendo, na kujadili kwa kina mada 12 muhimu zilizowasilishwa kuhusu uchaguzi.
“Washiriki wameonesha utayari wa kusimamia kwa ufanisi majukumu yao kwenye wilaya mbalimbali za Unguja, na sasa wana uwezo wa kutoa mafunzo kwa watendaji wa vituo,” alisema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, washiriki wa mafunzo hayo walitoa ahadi ya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, kufuata sheria na kuzingatia viapo vyao.
Mohammed Salim Hamad, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Mwanakwerekwe, alisema:
“Tumepata maarifa ya kutosha, tuko tayari kwa kazi ya kitaifa. Tutasimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria na tutakuwa waadilifu.”
Latifa Gharib Mgeni, Ofisa Msaidizi wa Uchaguzi kutoka Jimbo la Kiembe Samaki, na Maryam Haji Juma wa Jimbo la Malindi, walieleza kuwa watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia miongozo ya Tume na kutoa mafunzo sahihi kwa watendaji wa vituo ili uchaguzi uwe huru, wa haki na wa amani.
Kwa upande wake, Zawadi Saleh Ali kutoka Jimbo la Mwera alisema:”Sitaangusha Taifa. Nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi, nitatunza siri kama nilivyoapa.”
Kauli mbiu ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 ni “Kura yako, haki yako – Jitokeze kupiga kura”, ikisisitiza wajibu na haki ya kila raia kushiriki katika ujenzi wa demokrasia kwa njia ya kura.