Na Fauzia Mussa
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Dk. Haroun Ali Suleiman, amesema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa wasaidizi wa sheria katika kuimarisha utulivu na kudumisha amani nchini.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria yaliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni, Mjini Unguja, Dk. Suleiman alisema juhudi za wasaidizi wa sheria zimesaidia kuifikia jamii kwa kutoa elimu ya kisheria na huduma muhimu ambazo zinasaidia kuondoa migogoro na kulinda haki za wananchi.
“Wasaidizi wa sheria wamekuwa wakijitolea kutumia muda wao kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii. Huduma hii inasaidia kudumisha utulivu na kutunza amani iliyopo nchini. Serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwapatia nyenzo na mazingira bora ya kazi,” alisema Waziri Suleiman.
Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, pamoja na kuhakikisha kila msaidizi wa sheria anapata nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kuwapatia mafunzo na vifaa vinavyohitajika.
Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu, aliwataka wasaidizi wa sheria kutumia nafasi waliyonayo kueneza ujumbe wa amani na kuhamasisha utulivu, huku akiwataka wakuu wa wilaya kutoa ushirikiano kwa kutoa nafasi katika ofisi zao kwa ajili ya utoaji wa huduma hizo.
“Amani ni msingi wa maendeleo. Bila amani hakuna kinachoendelea. Tunapaswa kuilinda kwa nguvu zote,” aliongeza Dk. Suleiman, huku akimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapindunzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuwa kinara wa kuendeleza Amani na mshikamano Nchini.
Kwa upande wake, Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Harouna Mustafa Matata, alisema kuwa wizara hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na huduma za msaada wa kisheria.
Matata alibainisha kuwa kupitia juhudi hizo, zaidi ya watu 400,000 wamefikiwa Zanzibar huku zaidi ya wasaidizi wa sheria 238 wakishirikiana kutoa msaada huo visiwani.
Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria, Hanifa Ramadhan Said, alisema kuwa katika wiki ya msaada wa kisheria mwaka huu, wananchi 12,403 walifikiwa kupitia njia mbalimbali ikiwemo mashuleni, madrasa, viwanja vya michezo na hata kwa watu wenye ulemavu Unguja na Pemba.
Alifahamisha kuwa Maadhimisho hayo pia yalipambwa na shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo bonanza la mbio za ngalawa, kampeni za uelimishaji kwa jamii, na midahalo kupitia vyombo vya habari.
Ofisa Mradi kutoka Legal Services Facility (LSF), Bakar Hamad, aliishukuru Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria kwa kushirikiana nao, na kuiomba Serikali kutenga nafasi katika majengo ya mapya ya Mahakama za Wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kila wilaya.
“Ni muhimu kuwa na wakalimani wa lugha ya alama Katika Kazi zetu ili hata watu wenye ulemavu wa uziwi wapate haki zao kupitia huduma hizi,” alisema.
Mwakilishi wa watoa msaada wa kisheria, Shaaban Sarboko Makarani, alieleza kuwa licha ya juhudi za Serikali, bado wasaidizi hao wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa ofisi na vifaa, hali inayokwamisha utoaji wa huduma kwa ufanisi.
Alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kusaidia huduma hizo kuwa endelevu.
Maadhimisho ya mwaka huu yalibeba kaulimbiu isemayo: “Nafasi ya Watoaji wa Msaada wa Kisheria katika Kukuza na Kulinda Amani na Utulivu Zanzibar”, yakilenga kuonesha umuhimu wa huduma hiyo katika kuhakikisha jamii inaishi kwa amani na haki.