Kamishna wa Uhifadhi – TANAPA, CPA Musa Nassoro Kuji, ameongoza hafla ya kumuapisha rasmi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – Cecilia Mtanga leo Julai 18, 2025 Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha. Uapisho huo ni baada ya Kamishna huyo kuteuliwa na Bodi ya Wadhamini – TANAPA katika kikao cha 210 kilichofanyika jijini Mwanza Mei, 2025.
Katika hafla hiyo Kamishna Kuji alimpongeza Kamishna Mtanga kwa uteuzi huo sanjari na kuwa Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu – TANAPA na kumtaka aendeleze juhudi za kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili kwa weledi, uwajibikaji na moyo wa kizalendo. Aidha, amesisitiza mshikamano kwa watumishi wote katika kuhakikisha malengo ya TANAPA yanafikiwa kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi – Cecilia Mtanga aliishukuru Bodi ya Wadhamini – TANAPA kwa kumuamini na kumteua, hivyo ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa bidii na kushirikiana na wenzake ili kuhakikisha urithi wa taifa unasimamiwa ipasavyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo.