Wanawake wilayani Ubungo, wametakiwa kuungana mara baada ya kumalizika zoezi la uchaguzi wa ndani wa kura za maoni za udiwani viti maalum.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Uwt wilaya ya Ubungo, Samina Mashauri, wakati anafungua Mkutano Mkuu Maalum wa Uwt wilaya katika uchaguzi wa kura za maoni kwa madiwani wa viti maalum wa tarafa ya Magomeni jimbo la Ubungo, na tarafa ya Kibamba jimbo la Kibamba, uliofanyika katika shule ya sekondari ya wasichana ya Dar es salaam.
Samina, amebainisha kuwa wanawake ni nguzo kubwa ya ushindi wa CCM na Ushindi wa wagombea wa CCM nafasi ya Urais kwa Mwanamke mashuhuri Dokta Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti huyo wa Uwt wilaya, amewataka wajumbe wa mkutano Mkuu Maalum, kuchagua madiwani wanawake wataokua tayari kubeba kero za wanawake, kufanya kazi kwa kasi, ari na kujituma ili kuwasaidia wanawake wa makundi yote kwenye jamii.
Aidha Mwenyekiti Samina ametumia nafasi hiyo kuwasihi wanawake kupendana, kuheshimiana, na kusamehe pale walipokwanzana, katika kutafuta kura na wawe tayari kutafuta kura za ushindi wa CCM na Dokta Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi Mkuu.
Huku akiwataka wagombea kutulia kwani vikao vya uchujaji vitaendelea baada ya kura za maoni hivyo wagombea wote atayeongoza kura na asiyeongoza kura watabaki kuwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
Nae msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo kutoka ngazi ya Mkoa, Ambaye pia ni Katibu wa CCM wilaya ya Kigamboni Stanley Mkandawile amewasisitiza wajumbe na wagombea hata kama mgombea atashinda lakini ikaonekana katika vikao vinavyofuata alikuwa na sifa za kuvunja taratibu za uchaguzi basi jina lake linaweza lisirudi.
Mkutano Mkuu Maalum wa Uwt wilaya ya Ubungo umejumuisha majimbo mawili ya uchaguzi, Ubungo na Kibamba huku wajumbe wa mkutano huo waliopiga kura ni 1438 kati 1632, kutoka katika kata 14.
Mikutano ya Uwt iliyoanza kufanya uchaguzi wa kura za maoni za CCM, imeanza kwa kuzingatia mabadiliko yaliyofanywa na Mkutano Mkuu Maalum ulioongeza wapiga kura ambao ni wajumbe wa kamati za utekelezaji kwa ngazi ya kata na matawi.