Na Sophia Kingimali.
Kuelekea katika kumbukizi ya miaka 26 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Shirika la utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais , Tawala za Mikoa na Serikali za Mtaa(TAMISEMI) na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wameandaa shindano la insha
Wito umetolewa kwa wanafunzi kushiriki katika shindano hilo huku washiriki wakitakiwa kutokutumia udanganyifu katika kuandika insha hizo kwa kutumia akili unde (AI) na kueleza watakaofanya hivyo watagunduliwa na kuondolewa katika shindano hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam leo Julai 22,2025 Mkurugenzi wa Huduma za Televisheni wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Happiness Ngasala, amesema lengo la shindano hilo la insha ni kumuenzi Hayati Mwalimu Nyerere kwa mambo mazuri aliyoyafanya katika uhai wake.
Amesema shindano la insha ya Mwalimu Nyerere limeanza rasmi Julai 22 ,mwaka huu na linatarajia kuhitimishwa Oktoba 14,mwaka huu ,huku likibebwa na mada ya maadui wetu ambao ni Ujinga, Maradhi na Umasikini mambo ambayo yalishika hatamu katika Uongozi wake.
“Katika kumbukizi ya miaka 26 ya kifo cha baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tumeamua kuandaa shindano hili ambalo litahusisha wanafunzi kutoka shule za sekondari bara na visiwani kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita watayaeleza mambo mbalimbali aliyoyafanya Hayati Mwalimu Nyerere kupitia mfumo wa Isha kupitia mada ya maadui watatu ambao ni ujinga,maradhi na umasikini “Amesema Ngasala
Amesema washindi watano katika shindano hilo watapewa zawadi mbalimbali ikiwemo kompyuta mpakato, vyeti pamoja na fedha taslimu.
“Ili kutokomeza ujinga mageuzi ya elimu yaliofanyika na Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa elimu yetu lazima ijenge moyo wa kujitokeza kwa jamii nzima na kuwasaidia wanafunzi kukubali mabadiliko yanayoendana na maisha yetu badala ya yale ya kikoloni”amesema
Akizungumzia maandalizi amesema yamekamilika na mada ya shindano hilo zitasambazwa katika shule zote za Tanzania Bara na Visiwani .
Katika hatua nyingine Ngasala amesema mbali na uandishi wa Insha kwa wanafunzi pia TBC imeandaa mbio zitazojulikana kama ‘Mwalimu Nyerere Marathon’ zitakazofanyika Oktoba 14,mwaka huu Mkoani Mbeya ikiwa ndio kilele cha kumbukizi ya kifo hicho.
Pia amesema katika Kilele hicho kutakuwa na wiki ya vijana ambayo itahusisha shughuli mbalimbali za kijamii.