Na Pamela Mollel, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenan Kihongosi, ametoa wito kwa watoa huduma wa saluni jijini Arusha kuwa na mshikamano na kuonesha upendo mahali pa kazi badala ya kuendeleza fitina, wivu na majungu yanayoweza kudumaza maendeleo ya sekta hiyo.
Akizungumza Julai 22, 2025 na watoa huduma za saluni wakiwemo wasusi, vinyozi, wapaka rangi kucha na wataalamu wa masaji, Mhe. Kihongosi alisema hakuna sababu ya wafanyakazi kuhujumiana kwa sababu ya mafanikio au mvuto wa wenzao.
“Ukiona mwenzako kapendeza au kapata maendeleo kidogo, usiwe na kijicho. Tumeletwa hapa duniani kwa mfano wa Mungu. Hakuna haja ya kumchukia au kumchongea mwenzako kwa boss ili uonekane bora,” alisema Kihongosi.
Aidha, aliwakumbusha watoa huduma hao kutumia vipato vyao katika shughuli za maendeleo badala ya kujiingiza kwenye matumizi yasiyo na tija ambayo huishia kuwakatisha tamaa kimaisha.
Katika kikao hicho, RC Kihongosi alisikiliza malalamiko kutoka kwa mjasiriamali Bi. Rose Barage ambaye alieleza kuwa anapata manyanyaso kutoka kwa mtu anayeitwa Lusekelo, anayemkodisha chumba kwa bei ya juu licha ya kuwa ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Bi. Rose alidai kuwa pamoja na kulipa kodi kwa wakati, bado anakumbana na vitisho na maneno ya kejeli ambayo yanamnyima amani kazini kwake.
Kutokana na malalamiko hayo, Mhe. Kihongosi alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kumpatia Bi. Rose mkataba rasmi siku hiyo hiyo, ili kumlinda dhidi ya manyanyaso na kuendesha biashara kwa utulivu.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka watendaji wa jiji la Arusha kufuata sheria, taratibu na miongozo katika utendaji wao na kutengeneza mazingira bora kwa wafanyabiashara wadogo badala ya kuwabughudhi au kuwadhulumu haki zao.