


Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji Tanzania (CMT) Dkt. Martin Kolikoli akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24, 2025 jijini Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa elimu ya fedha
pamoja na kufanya uwekezaji katika masoko ya mitaji ya dhamana na namna bora ya kutatua migogoro ya kifedha itakapojitokeza, kwa ajili ya kupata haki.



Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano na Msajili wa Baraza la Masoko ya Mitaji Tanzania (CMT)
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Baraza la Masoko ya Mitaji Tanzania (CMT) limewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa ya kupata elimu ya fedha kutoka katika vyanzo sahihi, ili kuwasaidia kufanya uwekezaji katika masoko ya mitaji ya dhamana pamoja na kujua namna bora ya kutatua migogoro ya kifedha itakapojitokeza, kwa ajili ya kupata haki zao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24, 2025 jijini Dar es Salaam, Msajili wa Baraza hilo, Dkt. Martin Kolikoli, amesema kuna uhitaji mkubwa wa elimu ya fedha kwa Watanzania ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uwekezaji wa dhamana.
“Watanzania wanapaswa kujifunza kuhusu maeneo sahihi ya kuwekeza katika masoko ya mitaji ya dhamana, na pia kufahamu namna ya kutatua migogoro ya kifedha kwa kufuata mifumo rasmi. Elimu ya fedha ni msingi wa maamuzi bora ya kifedha,” amesema Dkt. Kolikoli.
Ameongeza kuwa Baraza la Masoko ya Mitaji ni chombo maalum kilichoundwa kusikiliza na kutatua migogoro inayohusiana na sekta ya dhamana, hivyo ni vyema wananchi wakalitambua na kulitumia kwa manufaa yao.
“Sasa Baraza lipo, na ni sehemu rasmi ya kushughulikia migogoro ya sekta ya dhamana. Tunawakaribisha Watanzania kuendelea kujifunza kuhusu majukumu ya CMT na nafasi yake katika kuendeleza masoko ya mitaji hapa nchini,” ameongeza Dkt. Kolikoli.
Aidha, Dkt. Kolikoli amesisitiza kuwa huu ni wakati muafaka kwa Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika uwekezaji, lakini akawaasa kuhakikisha wanapata elimu kutoka kwa watu na taasisi sahihi kabla ya kuwekeza.
Baraza la Masoko ya Mitaji linalenga kukuza maarifa ya kifedha kwa umma, kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu huduma zake, na kuanzisha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha usajili na ufuatiliaji wa kesi mbalimbali za madai katika sekta ya dhamana.
CMT ni taasisi huru ya haki ya madai iliyoanzishwa chini ya Kifungu cha 136A(1) cha Sheria ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (Sura ya 79 ya Sheria za Tanzania), ikiwa na jukumu la kuhakikisha uwazi, usawa, na haki vinazingatiwa katika sekta ya kifedha nchini.