Na John Bukuku, Kibaha
Kampuni ya Xinghao Group Company Ltd kupitia chapa yake ya Lulu Cement, imekabidhi msaada wa madawati 200 na shilingi milioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa fenicha za walimu katika Shule ya Msingi Misugusugu, iliyopo Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani.
Msaada huo una thamani ya shilingi milioni 36, ukilenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi na walimu shuleni hapo.
Makabidhiano hayo yalifanyika Julai 25, 2025 ambapo Meneja wa kiwanda hicho, Bw. Wan Jianguo, alisema waliguswa na changamoto ya uhaba wa madawati walipofanya ziara ya kutembelea shule hiyo.
Alisema kuwa serikali imefanya kazi kubwa ya kuweka miundombinu bora ya shule, na wao kama wawekezaji wanaona ni wajibu kuchangia kwenye nyanja ya vifaa vya msingi vya elimu.
“Tunatambua kuwa maendeleo ya elimu ni jukumu la kila mmoja wetu, na sisi tunajivunia kuwa sehemu ya mabadiliko haya chanya,” alisema Jianguo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Mwl. Theresia Kyara aliishukuru kampuni hiyo kwa mchango mkubwa unaosaidia kupunguza changamoto zilizopo shuleni.
Alisema msaada huo utapunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kuongeza ari ya ufundishaji kwa walimu, hivyo kuongeza ufaulu wa wanafunzi.
Mwl. Kyara aliwahakikishia wafadhili kuwa vifaa hivyo vitatumika kama ilivyokusudiwa na kuwa mali ya kudumu kwa shule hiyo.
Pia aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji yanayowavutia wadau kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na wananchi wa eneo hilo waliopata fursa ya kushiriki hafla hiyo walieleza kufurahishwa na msaada huo na kuahidi kuutunza.
“Tunaahidi kuwa walinzi wa vifaa hivi kwa kuhakikisha vinadumu kwa muda mrefu na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa,” alisema mmoja wa wazazi waliokuwepo.
Wameeleza kuwa ushirikiano wa aina hiyo kati ya sekta binafsi na jamii ni mfano wa kuigwa katika kuleta maendeleo kwenye maeneo ya elimu, afya na miundombinu.
Hafla hiyo ya makabidhiano ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa elimu, wawakilishi wa kampuni na wananchi, ikiwa ni ishara ya mshikamano wa pamoja katika kuinua sekta ya elimu nchini.