Ushirikishaji wakandarasi wazawa ambao umeenda sambamba na kuwatumia vijana wa Tanzania katika kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji umetoa fursa ya maarifa mapya na uzoefu katika suala la ujenzi wa miradi.
Vibarua wanaotekeleza mradi wa maji wa miji 28 mjini Chato wamesema hayo wakiongea na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) wakati akikagua mradi huo.
Bw. Mengi Mtindo ambaye ni fundi na mkazi wa Chato akiwawakilisha wenzake wanaofanya kazi ya kibarua katika mradi wa maji wa miji 28 Chato amesema hivi sasa wanayo maarifa ya kutosha ya kutekeleza miradi ya maji na kuishukuru Serikali kwa kuwapa kipaumbele.
“Mheshimiwa Waziri tunashukuru sana kwa maarifa ambayo sasa tunayo katika utekelezaji wa miradi ya maji. Tangu mradi huu ulipoanza tumekuwepo. Tumepewa kipaumbeke katika ajira. Sasa tuko tayari kujiendesha wenyewe hata hawa wakandarasi wa kigeni wakiondoka.” Mengi amesema huku akishangiliwa na wenzake.
Waziri Aweso ambaye aliambatana na Katibu Mkuu Mhandisi Mwajuma Waziri katika ukaguzi huo amewahakikishia kuwa serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wazawa katika utekelezaji wa miradi ili kuongeza maarifa zaidi. Amesisitiza kuwa adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muunganoa wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wazawa wanawezeshwa ili kupata wataalam ambao wataweza kusimamia na kuendesha miradi ya serikali.
Mradi wa maji wa miji 28 mjini Chato unatekekezwa na kampuni ya M/s Afcons Infrastructure Limited chini ya Mtaalamu Mshauri WAPCOS LIMITED kampuni kutoka India.
Mradi utawezesha upatikanaji wa maji katika mji wa Chato kufika lita milioni 14 kwa siku wakati mahitaji kwa sasa ni lita milioni 8 kwa siku. Hivi sasa uzalishaji ni lita milioni 4 kwa siku.