Babati Julai 25, 2025
Mahakama ya Wilaya ya Babati imemtia hatiani aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Zahanati ya Endagwe, Bw. Mohamed Twalib Baya, kwa kosa la kughushi na kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi milioni 8.015.
Katika shauri la Uhujumu Uchumi Na. 15921/2025, lililosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Victor Kimario, imethibitika kuwa mshtakiwa alighushi sahihi za watia saini katika akaunti ya Zahanati ya Endagwe na kutumia nyaraka hizo kuchukua fedha ambazo alizitumia kinyume na taratibu.
Mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kufanya makubaliano ya kukiri kosa (plea bargaining) na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), hatua iliyopelekea kupatikana kwa hukumu ya haraka.
Awali, Bw. Twalib alishtakiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(a), na 337 vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 (Marejeo ya 2022), pamoja na makosa ya ubadhirifu wa fedha chini ya Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, na kosa la kuisababishia mamlaka hasara kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza sambamba na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200.
Mahakama imemhukumu kulipa faini ya shilingi 200,000 au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela, pamoja na kurejesha fedha zote alizozifanyia ubadhirifu.
Hadi hukumu hiyo inasomwa, mshtakiwa alikuwa amesharejesha shilingi milioni 4 kwenye akaunti ya Zahanati ya Endagwe iliyopo benki ya NMB, huku akitakiwa kurejesha kiasi kilichobaki ndani ya mwezi mmoja.
Kesi hiyo iliendeshwa na waendesha mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Manyara ambao ni Neema Gembe, Davis Masambu, na Catherine Ngessy.