Na Alex Sonna, Dodoma
Serikali imedhamiria kuondoa ujinga kwa kasi nchini kupitia mafunzo maalum ya wawezeshaji wa elimu ya watu wazima yanayoshirikisha maafisa magereza na wataalam wa elimu.
Akizindua mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omary, amesema kuwa mafunzo hayo ni kwa ajili ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Magereza pamoja na wawezeshaji wa programu ya Kisomo yaliyofanyika jijini Dodoma.
Dkt.Omary amesema kuwa Tanzania, ambayo ilipiga hatua kubwa kufuta ujinga miaka ya 90, bado ina changamoto kubwa ambapo kwa mujibu wa sensa ya 2022, takribani asilimia 17 ya Watanzania hawana stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
“Mafunzo haya yanalenga kupunguza pengo hili na kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu na ujuzi wa maisha,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali imeanzisha vituo vya kisasa vya mafunzo na karakana za amali, sambamba na mbinu mpya ya RIFLEKTI inayochanganya elimu ya KKK na stadi za maisha ili kuwajengea wananchi uwezo wa kujitegemea kiuchumi.
Amesema ushiriki wa maafisa magereza ni hatua muhimu katika kuwafikia wafungwa na walioko kwenye vituo vya urekebu, lengo likiwa kuwabadilisha kuwa raia wema wenye mchango kwa taifa.
Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Philipo Sanga, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya taasisi hiyo na ni maandalizi ya kampeni kubwa ya madarasa ya kisomo. “Tunajenga kizazi kipya kinachoweza kushindana katika soko la ajira, kupambana na umaskini na kuchangia pato la taifa,” alisema Prof. Sanga.
Mafunzo hayo yamekusanya viongozi wa elimu wa mikoa na wilaya, wataalamu wa elimu ya watu wazima na maafisa magereza kutoka mikoa mbalimbali nchini, yakilenga kuimarisha uhamasishaji wa elimu nje ya mfumo rasmi na kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.