Na John Bukuku, DAR ES SALAAM
Julai 31, 2025
Katika tukio lililofanyika leo jijini Dar es Salaam, Kampuni ya kimataifa ya FUCHS Lubricants Tanzania Limited imezindua rasmi bidhaa yake mpya ya vilainishi vya injini kwa pikipiki na bajaji iitwayo TITAN MAX 4T SL 20W50 – oili ya daraja la juu iliyobuniwa mahsusi kuongeza ufanisi na kudumu kwa muda mrefu kwa vyombo vya usafiri vinavyotegemewa na Watanzania wengi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja Fedha wa FUCHS Tanzania, Bw. Taalib Shariff, alisema kuwa kwa muda mrefu wamiliki wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji wamekuwa wakipoteza mapato kutokana na uharibifu wa mara kwa mara wa injini. Alibainisha kuwa FUCHS – kampuni yenye makao makuu nchini Ujerumani – imeliona hilo kama changamoto kubwa na hivyo kufanya tafiti za kina zilizochangia kuzalishwa kwa TITAN MAX 4T SL 20W50 kama suluhisho la muda mrefu.
“Tulizingatia mazingira ya Kiafrika ikiwemo joto kali, vumbi, na matumizi ya aina mbalimbali za mafuta katika soko la ndani. Hii ni hatua kubwa katika kuhakikisha madereva wanaendesha kwa uhakika bila hofu ya injini kuharibika,” alisema Shariff.
Aidha, alieleza kuwa kampuni hiyo tayari ina wateja wengi wa viwandani na inasambaza bidhaa zake katika mikoa mbalimbali kama Arusha, Mwanza, na mingineyo. Aliongeza kuwa hivi karibuni FUCHS inatarajia kufungua tawi jipya mkoani Dodoma, jambo ambalo litawarahisishia wateja kupata huduma kwa ukaribu zaidi.
Oili ya TITAN MAX 4T SL 20W50 imetengenezwa kwa malighafi safi daraja la pili na imekidhi viwango vya juu vya kimataifa, ikiwa ni pamoja na API SL na SAE 20W50. Kilainishi hiki hufanya kazi nne kuu muhimu kwenye injini, ambazo ni:
Kwa mujibu wa wataalamu wa FUCHS, matumizi ya oili hiyo yatasaidia madereva kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara Kulainisha maeneo yenye msuguano, Kuzuia kutu na mmomonyoko, Kusafisha injini dhidi ya uchafu na Kuipoza injini na kuongeza ufanisi pia kuongeza muda wa uendeshaji, na hivyo kuongeza kipato.
“Tumeitengeneza TITAN MAX 4T SL 20W50 kwa ajili ya kuondoa kabisa usumbufu unaowakumba wamiliki wa pikipiki na bajaji. Kwa kutumia bidhaa hii, utatoka karakana na kwenda moja kwa moja kuisaka noti,” alisema mmoja wa wahandisi kutoka FUCHS.
Kampuni hiyo imewahimiza madereva kote nchini kuchagua TITAN MAX 4T SL 20W50 kama njia sahihi ya kujiinua kiuchumi na kuepuka matatizo ya kiufundi yanayosababishwa na vilainishi visivyo na viwango.