DAR ES SALAAM: KAMISHENI ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imeingia mkataba wa miaka mitatu wa ushirikiano na Hospitali ya Haitech Sai kwa lengo la kuhakikisha mabondia nchini wanapata huduma za afya kabla na baada ya mapambano yao.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Mwenyekiti wa TPBRC, Emmanuel Salehe amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu kwa mabondia kufahamu afya zao kwa wakati, ikiwa ni pamoja na vipimo vya afya vya kabla na baada ya pambano pamoja na kipimo cha kudhibiti matumizi ya dawa na mbinu haramu michezoni (anti-doping).
“Huu ushirikiano unasaidia mabondia wetu kufahamu afya zao. Tumeamua kujali afya na usalama wa wanamichezo wetu, hasa ukizingatia mchezo huu ni wa kugusana, hivyo tunahitaji uchunguzi wa kina,” amesema Salehe.
Salehe ameongeza kuwa moja ya changamoto waliyoibaini ni kutokuwepo kwa rekodi za afya za mabondia wengi, jambo ambalo Haitech Sai inaweza kusaidia kulitatua, hasa katika kutambua matatizo ya kiafya kama vile ya mikono ambayo ni sehemu muhimu kwenye mchezo wa ngumi.
“Kwa kuwa ngumi ni mchezo hatarishi, jambo la afya na usalama kwa mabondia wetu ni la kipaumbele. Tunaamini Haitech Sai itatusaidia kufanikisha hilo,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Hospitali ya Hitachi Sai, Gean Cabral alisema wamefurahishwa na nafasi ya kushirikiana na TPBRC, na watahakikisha mabondia wanapata huduma bora za kiafya katika vipindi vyote muhimu kabla na baada ya mapambano.
“Tulikuwa na ushirikiano na michezo mingine kama kriketi, lakini sasa tuna furaha kuungana na TPBRC ili kusaidia mabondia kufahamu afya zao na kuwa salama wanaposhiriki mashindano,” amesema Cabral.
The post TPBRC yawakumbuka Mabondia, yawapa Hospitali first appeared on SpotiLEO.