NA DENIS MLOWE, MAFINGA
KATIKA kuelekea kura za maoni za watia nia wa Jimbo la Mufindi Kaskazini ambao wameonyesha mvuto kwenye jimbo hilo kutokana na uwasilishaji wa hoja zake ni mgombea Godfrey Ngupula.
Ngupula ambaye katika kura za maoni za mwaka 2020 alishika nafasi ya pili, amekuwa kivutio kutokana na manjonjo huku akiwasilisha hoja kwa umakini kuweza kuteka nyoyo za wajumbe wampe kura.
Akizungumzia ahadi zake katika jimbo hilo alisema kuwa atashughulikia changamoto ya barabara inayolalamikiwa kwa muda mrefu, huku akisema jimbo hilo limekosa sahihi wa kujua siri kutatua changamoto hiyo ambapo yeye anazo.
Alisema kuwa barabara muhimu ikiwemo ile ya Mdabulo na ile ya Kinyanambo hadi Madibira, zimeendelea kuwa kero kwa wananchi, hali inayokwamisha maendeleo hivyo endapo watampa ridhaa atahakikisha changamoto hiyo inaisha.
Ngupula alisema uzoefu wake wa uongozi ni chachu ya kutatua changamoto hizo, akitaja sifa tatu kuu za kiongozi alizonazo kuwa ni upendo, uwezo wa kutekeleza mambo magumu na ustahimilivu.
Alisema aliaminiwa na Rais kushika nyadhifa serikalini ikiwemo kuwa Mkuu wa Wilaya na Mhifadhi Mkuu wa Bahari katika hifadhi za bahari na maeneo tengefu nafasi anayosema imemjengea uwezo wa kupanga na kusimamia miradi mikubwa ya maendeleo.
Amesema iwapo atapata ridhaa ya wananchi kupitia kura za maoni ndani ya CCM na baadaye uchaguzi mkuu, ataweka kipaumbele kwenye ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kuboresha huduma za kijamii na kuhamasisha miradi ya uchumi inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.