Na John Jayros
MTIA nia wa Ubunge jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa ameweka vipaumbele endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo huku akisisitiza uwekezaji mkubwa unaokuja katika jimbo hilo lazima uwanufaishe wananchi wa Rufiji.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa kata ya Ngarambe na Utete, Mhe. Mchengerwa amesema kutokana na kazi kubwa aliyofanya kwa kushirikiana na Serikali na wananchi katika kipindi chake tayari wawekezaji wengi wameonyesha nia ya kuwekeza Rufiji kilichobaki ni kusimamia namna bora ya kuwashirikisha wananchi ili wanufaike na uwekezaji huo kwa kupata ajira.
“Hadi sasa kwa jitihada tulizozifanya mimi na Serikali yetu matunda yameanza kuonekana kwani tayari wawekezaji wakubwa katika eneo la viwanda vikubwa wameomba kuja kuwekeza kilichobaki ni kusimamia ili tuweze kuwapa fursa za ajira ambazo wameshaahidi kuzitoa kwa vijana na akina mama”. Amefafanua Mhe. Mohamed Mchengerwa
Amesema katika kipindi chote akiwa Mbunge wa Rufiji amebeba ndoto na maono ya wananchi wa Rufiji za kuwa na maisha bora kwa kufanya kazi kwa bidii, ambapo tayari mapinduzi makubwa ya fikra na uchumi yamejitokeza.
Aidha, amehoji kuwa wawekezaji wapo wengi, lakini jamii inanufaika kiasi gani na kusisitiza kwamba ni lazima vijana na wanawake wapate ajira zenye staha, pia wawekezaji waliojitokeza wazingatie sheria za kazi kwa maslahi mapana ya wanarufiji.
Ametaja baadhi ya uwekezaji unaotarajiwa kufanyika na idadi ya ajira zitakazopatikana kuwa ni pamoja na kiwanda kikubwa cha sukari kinachotarajia kuzalisha ajira 6000.
Vingine ni kiwanda cha ndizi chenye mtaji wa zaidi ya shilingi trioni 1.5 kitakachotoa ajira 1000 kila siku na kiwanda kikubwa cha mafuta ya mawese kitakachojengwa eneo la Chumbi kitakachotoa ajira 6000 kwa akina mama.
“Sitafuti nafasi, nataka maendeleo nagombea kwa sababu ya dhamira, si maslahi binafsi naomba kusisitiza kuwa katika kipindi chote cha ubunge wangu nimetanguliza mbele maslahi ya kuwaletea maendeleo wananchi wangu katika sekta zote ikiwa ni pamoja na elimu, afya, miundombinu, maji na kilimo”. Amefafanua Mhe. Mchengerwa
Akitoa mfano amesema ya baadhi ya maeneo katika Sekta ya Afya kumekuwa na ongezeko la toka zahanati 20 hadi 42 na vituo vya afya 3 hadi 9 na magari ya kubebea wagonjwa toka 2 hadi 7.
Kwa upande wa elimu kumekuwa ongezeko la wanafunzi wa shule za Msingi kutoka 2000 hadi 12000 wakati kwenye umeme vijiji vyote 38 vimepatiwa kutoka vijiji sita tu vya awali.
Naye mtia nia mwingine Mwalimu Selemani Mhekela amesema kwa upande wake endapo atachaguliwa atashirikiana na wananchi kutokomeza rushwa.
Aidha, Hamisa Kisoma anayegombea pia katika jimbo hilo ameahidi kuwaletea maendeleo ambapo ameomba akopeshwe imani.
Naye Salma Hamisi amesema atapigania asilimia 10 za fedha zinazotengwana Serikali kwa ajili ya vijana, wanawake na wenye ulemavu ili ziwanufaishe.