DAR ES SALAAM, AGOSTI 04, 2025
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini ikiwemo vyombo vya habari kushirikiana kwa dhati kulinda Watoto na vijana ili kuendelea kubaki na hazina yenye tija katika taifa letu.
IGP Wambura ametoa wito huo Jijini Dar es salaam wakati akizindua kampeni ya Tuwaambie kabla hawajaharibiwa awamu ya pili yenye lengo la kuwakumbusha vijana kujitambua na kuchukua tahadhari kabla hawajaharibiwa na kujiingiza katika vitendo visivyofaa.
Aidha, IGP Wambura amewataka Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto kote nchini kuendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha kuwa malengo ya kampeni hiyo yanaifikia jamii ili kujenga taifa bora.
Kwa upande wake Kamishna wa Polisi Jamii, Faustine Shilogile amesema kamisheni hiyo itaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinakoma nchini huku akiwapongeza watendaji hao kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia katika jamii ya watanzania