Klabu ya Yanga SC imekubaliana na Al Sadd SC ya Qatar kuhusu uhamisho wa mshambuliaji wake nyota, Clement Mzize, kwa ada inayozidi Shilingi bilioni 2, lakini dili hilo limekwama kutokana na madai ya mshahara kutoka kwa mchezaji huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa wakati Yanga ikiwa tayari kumruhusu Mzize kujiunga na miamba hiyo ya Qatar, upande wa mchezaji umeweka ngumu baada ya kugomea mshahara wa TZS milioni 75 uliotolewa na Al Sadd, akisisitiza anataka kulipwa TZS milioni 124 kwa mwezi.
Mvutano huo kuhusu maslahi binafsi ya mchezaji sasa umeweka hatihati mustakabali wa uhamisho huo, huku mazungumzo kati ya pande zote yakiendelea ili kufikia muafaka.
Mzize, ambaye kwa sasa ni miongoni mwa washambuliaji bora wa kizawa akiwa na umri mdogo zaidi (Miaka 21), ameibua mvuto mkubwa kutokana na kiwango chake kizuri ndani na nje ya ligi ya Tanzania.