Muimbaji na muigizaji maarufu wa Bongo, Lulu Abas almaarufu Lulu Diva, ameamua kufunguka kwa mara ya kwanza kuhusu tukio la kusikitisha na la aibu lililomkumba—picha zake za utupu kusambazwa mitandaoni.
Akizungumza akiwa mgeni katika kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM, Lulu ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea baada ya mpenzi wake wa zamani, mwanaume mwenye umri wa zaidi ya miaka 50 aliyekuwa anaishi Uingereza, kuvujisha picha hizo kama njia ya kulipiza kisasi baada ya kuachwa.
“Nilijua vijana wameshaniumiza sana, nikasema nijitulize kwa mtu mzima, kumbe naye ana matatizo ya kisaikolojia,” amesema Lulu Diva kwa sauti ya kujiamini lakini yenye huzuni iliyofichika.
Lulu amesema kuwa picha hizo zilichukuliwa wakati wa mawasiliano yao ya video call, kipindi ambacho alikuwa na imani kubwa na mpenzi wake huyo kiasi cha kuweza kuzungumza naye hata akiwa bafuni. Lakini mambo yalibadilika walipoachana, ndipo mwanaume huyo alipoamua kuzisambaza mtandaoni.
“Picha zilivujishwa baada ya mimi kumkataa, ilinitesa hadi nikanywa sumu,” alieleza Lulu kwa uchungu.
Tukio hilo limezua mjadala mpana kuhusu usalama wa faragha katika mahusiano ya kimapenzi, hasa yale yanayofanyika kwa njia ya kidigitali. Limeibua maswali kuhusu uaminifu, heshima na matumizi mabaya ya teknolojia katika mahusiano.
Lulu ametoa somo kwa jamii na mashabiki zake kuwa “Kamwe usiruhusu kupigwa picha za utupu au kuzituma kwa mpenzi wako, hata kama unampenda kiasi gani. Teknolojia inabadilika, lakini aibu ya picha hizo kusambaa haifutiki kirahisi.”
The post “Lulu Diva afunguka ishu ya kunywa sumu first appeared on SpotiLEO.