Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Bi. Rosemary Senyamule, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa juhudi kubwa inazozifanya katika kutoa elimu ya kisheria pamoja na huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi, kupitia ushiriki wake kwenye Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Akizungumza leo Agosti 5,2025 mara baada ya kutembelea banda la wizara hiyo,Bi. Senyamule amesema kuwa utoaji wa elimu na msaada wa kisheria ni hatua muhimu katika kuwawezesha wananchi kuelewa haki zao za kisheria na kujenga jamii inayozingatia utawala wa sheria.
“Nachukua fursa hii kuipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwafuata wananchi moja kwa moja na kuwapatia huduma hizi muhimu. Hii inaonyesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi haki, uelewa na usawa wa kisheria,” amesema Senyamule.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria wakati wa Maonesho hayo ili waweze kupatiwa msaada wa kisheria pamoja na elimu inayotolewa katika banda hilo.
Wizara ya Katiba na Sheria inashiriki maonesho haya kwa kutoa elimu na msaada wa kisheria bila malipo kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.