Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka kambi katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea mkoani Dodoma kwa lengo la kutoa huduma na elimu kwa wananchi, ikiwemo uelewa kuhusu madhara ya utakatishaji fedha katika uchumi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho hayo, Wakili Mkuu wa Serikali kutoka BoT, Bw. Stanford Mbengane, alisema Benki Kuu ina jukumu la kuhakikisha kuwa fedha zinazoingia kwenye uchumi wa Tanzania ni halali na salama kwa matumizi ya umma.
“BoT inafanya kazi ya kudhibiti utakatishaji fedha unaofanywa na watu wanaopata fedha kwa njia zisizo halali. Tunahakikisha fedha hizo haziingii kwenye mfumo rasmi wa kifedha, kwa kuwa zinachangia mfumuko wa bei na kuvuruga utulivu wa uchumi,” alisema Bw. Mbengane.
Aliongeza kuwa moja ya mikakati muhimu ya kupambana na utakatishaji fedha ni kuhakikisha watoa huduma za kifedha wanazingatia kikamilifu utaratibu wa kumtambua mteja (Know Your Customer – KYC), ikiwa ni pamoja na kubaini chanzo halali cha mapato ya mteja.
“Usalama wa mfumo wa kifedha unategemea uwezo wetu wa kuzuia fedha haramu kuingia kwenye mzunguko wa uchumi. Hii ndiyo sababu elimu kama hii ni muhimu kwa umma na watoa huduma wote wa kifedha,” alisisitiza.
BoT inatumia jukwaa la Nanenane kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwajengea uelewa wa masuala ya kifedha, sambamba na kuhimiza uwajibikaji katika matumizi ya fedha na ufuatiliaji wa vyanzo vya mapato vinavyoingia katika mfumo wa uchumi wa Taifa.