Aliyewahi kuwa Spika na aliyekuwa Mbunge wa Kongwa, Job Yustino Ndugai amefariki Dunia, leo Agosti 6, 2025, taarifa ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, Dkt. Tulia Ackson imeeleza kuwa msiba umetokea Dodoma
Dkt. Tulia amesema Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na Kamati ya Mazishi pamoja na familia ya Marehemu inaratibu mipango ya mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
WASIFU MDOGO WA JOB NDUGAI
Alizaliwa Januari 21, 1963 na kupata elimu ya msingi kutoka Shule ya Msingi Mtare kuanzia mwaka 1971-1977. Alianza elimu ya Sekondari ya Kibaha mwaka 1978-1981 na kumalizia Shule ya Sekondari Old Moshi kuanzia 1982-1984.
Amesoma Stashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori kutoka Chuo cha Mweka kuanzia mwaka 1986-1988, kisha Shahada ya Kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1989-1993).
Amesoma Post Graduate kutoka Chuo cha Kilimo nchini Norway kuanzia 1994-1995 na kusoma Shahada ya Umahiri kutoka chuo hicho (1995-1996).
Safari yake ya elimu iliishia Eastern and Southern African Management Institute ambapo alisoma Shahada ya Umahiri katika Usimamizi wa Biashara (2005-2008)
Amekuwa Mbunge wa Kongwa kwa miaka 25 .