Nane Nane, Dodoma
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), George Seni, amesema kuwa Serikali imetumia fedha nyingi kuzalisha vitambulisho vya taifa kupitia NIDA, lakini baadhi ya wananchi bado hawajachukua vitambulisho hivyo licha ya juhudi kubwa zilizofanywa katika kugawa.
Ametoa kauli hiyo katika mahojiano Maalum na Fullshangweblog Agosti 7, 2025, katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayofanyika kwenye Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Seni ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanachukua vitambulisho vyao ambavyo tayari vimezalishwa na viko tayari kuchukuliwa.
“Taasisi imefanya juhudi mbalimbali za kugawa vitambulisho kwa wananchi, lakini bahati mbaya sana baadhi ya wananchi hawajachukua vitambulisho,” amesema Seni.
Ameeleza kuwa mwezi Mei mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA alitangaza hatua ya kuzifungia namba za vitambulisho ambavyo havijachukuliwa, ambapo kulikuwepo na takriban vitambulisho 700,000. Hata hivyo, amesema kuwa zoezi hilo lilichochea mwamko kwa muda mfupi tu.
“Niwaombe sana Watanzania popote mlipo… kama unajua kwamba ukishapata namba ya kitambulisho, basi jitahidi ukachukue kitambulisho chako pale ulipojiandikisha,” aliongeza.
Seni amesema kuwa kwa wananchi walioko mbali na maeneo waliyosajiliwa, wanaweza kufika katika ofisi yoyote ya wilaya ya NIDA iliyo karibu na kueleza walikojiandikisha ili kusaidiwa kupata vitambulisho vyao.
“Naomba tena sana wananchi wote tujitahidi kuchukua vitambulisho vyetu… kila sehemu utakapotaka kufanya kazi yako yoyote, utaulizwa kitambulisho,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, George Seni ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi kutembelea banda la NIDA katika maonesho hayo ya Nanenane kwa mwaka huu wa 2025.
“NIDA imekuwa ikifanya kazi kwa karibu sana na taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kwa ujumla. Mtakumbuka hivi karibuni tulishiriki maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, ambapo tulifanya shughuli za utambuzi na uandikishaji wa wananchi,” amesema.
Amesema huduma walizotoa zimepokelewa vizuri na wananchi, huku viongozi mbalimbali wakionesha kuridhishwa na maboresho yaliyofanyika ndani ya taasisi hiyo chini ya uongozi wa Kamishna Jenerali Mstaafu, James Kaji.
“Ujio wa Mkurugenzi Mkuu huyu umeonyesha kwamba tunaelekea sehemu nzuri zaidi kutoka pale tulipokuwa,” amesema.
Aidha, George Seni ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuratibu vizuri maonesho ya Nanenane mwaka huu. Amesema maonesho ya mwaka huu yamefana sana, na kueleza kuwa wananchi wamekuwa wakifika kwa wingi kwenye banda la NIDA, kueleza matatizo yao na kupata huduma moja kwa moja au kupewa maelekezo ya kufika katika ofisi za wilaya.
“Wananchi wengi wametoa ushuhuda kwamba matatizo yao mengi yameweza kuhudumiwa hapa hapa na kutoka na suluhu,” amesema.
Mwisho, Seni amewakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda la NIDA katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ili kupata huduma mbalimbali za mamlaka hiyo.