KATIKA kambi ya mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwa sasa pale KMC Complex, ikijiandaa na msimu mpya wa mashindano kuna balaa la mastaa wapya wa timu hiyo ambao nilipata nafasi ya kuwaona wanakiwasha, lakini gumzo ni Moussa Bala Conte na Abdul-Nasir Mohammed ‘Casemiro’.
Kinara ni Conte ambaye akiwa katikati ya uwanja kuna kazi ya maana ameanza kuitambulisha. Conte aliyesajiliwa na Yanga akitokea CS Sfaxien ya Tunisia baada ya mabingwa hao wa soka Tanzania kuununua mkataba wake, anaonyesha shoo nzuri kwa ubora wa kupiga pasi tofauti lakini pia kukaba.
Tuanze na pasi zake ni kwamba jamaa anajua kupiga pasi ndefu ambapo anapokea na kushoto kisha kuitupa na kulia na ukimpa na kulia anaitupa ndefu kwa mguu wa kushoto
Kiungo huyo raia wa Guinea amekuwa hodari kwa kupiga pasi fupi na ndefu ambapo kwa mazoezi ya jana alitumia dakika 40 kupiga pasi 38 na ndani ya hizo ikapotea moja tu ambayo winga mpya wa timu hiyo Ofen Chikola aliichelewa kuinasa.
Achana na Conte kuna huyu bwana mdogo Abdulnassir Mohammed ‘Casemiro’ aliyesajiliwa kutoka visiwani Zanzibar, naye ana kijiji’ chake kwa ubora wake wa kukaba kwa nguvu.
Casemiro, ametumwa kukaba tu na akishaikamata mali basi anapambana kusogeza mashambulizi mbele akiwavutia wengi kutokana na kazi anayoifanya