Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina, akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maonesho ya Wakulima ya Nane Nane, Kanda ya Ziwa Magharibi, yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Na.Mwandishi Wetu.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kupitia maonesho ya Wakulima ya Nane Nane, Kanda ya Ziwa Magharibi, imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 300, wakiwemo waliowasilisha malalamiko mbalimbali yanayohusu huduma za umeme na maji.
Hayo yameelezwa Agosti 8, 2025 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina,wakati akizungumza na waandishi wa habari katika kilele cha maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.
Mhina amesema katika kipindi cha maonesho hayo , banda la EWURA lilitembelewa na wastani wa watu 40 hadi 50 kwa siku, waliopata huduma za elimu pamoja na fursa ya kuwasilisha changamoto zao.
“Tumepokea malalamiko mbalimbali, hasa kuhusu ucheleweshwaji wa kuunganishiwa umeme pamoja na matatizo kwenye ankara za maji. Baadhi ya changamoto tumeweza kuzitatua papo kwa papo,” amesema Mhina.
Ameongeza kuwa kupitia ushiriki huo, EWURA imeweza kuwafikia wananchi wa aina zote kutoka wale wenye kipato kikubwa hadi wa kipato cha chini ambao mara nyingi hawapati fursa ya kufika katika ofisi za mamlaka hiyo zilizopo mijini.
Mhina alibainisha kuwa EWURA imebaini baadhi ya changamoto zinazowakabili wananchi zingeweza kutatuliwa na watoa huduma kama TANESCO na mamlaka za maji iwapo zingetatuliwa kwa uwajibikaji wa karibu zaidi.
“Tuna mpango wa kufanya kikao cha pamoja na TANESCO na mamlaka zote za maji katika Kanda ya Ziwa kabla ya mwisho wa Septemba. Lengo ni kutoa semina elekezi kwa watoa huduma na wanasheria wao ili kukumbushana wajibu wao kwa wananchi,” alisema Mhina.
Aidha, alisema baadhi ya malalamiko yataanza kufanyiwa kazi kuanzia wiki inayofuata, na kusisitiza kuwa EWURA itaendelea kuhakikisha watoa huduma wanazingatia viwango vya ubora na utoaji wa huduma kwa mujibu wa sheria.
Mhina pia alisema ushiriki wa EWURA katika maonesho hayo umetimiza moja ya majukumu yake ya msingi ya utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika kupata huduma bora za nishati na maji.
“Kupitia majukwaa kama haya, tunatoa elimu ya moja kwa moja kwa wananchi kuhusu namna ya kushughulikia changamoto zao, taratibu za kupata huduma, pamoja na kuelewa wajibu wa mtoa huduma,” aliongeza.