NAIROBI: KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) imekutana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu nidhamu katika michuano ya CHAN inayoendelea na kutoa uamuzi dhidi ya Morocco.
Katika kikao hicho, Shirikisho la Soka Morocco (FRMF) limetozwa faini ya dola za kimarekani 5,000 sawa na zaidi ya sh milioni 12 kutokana na tabia isiyofaa ya wachezaji katika mechi dhidi ya Kenya.
Aidha dola 2,500 zimewekwa kando kwa sharti kuwa kosa kama hilo halitarudiwa katika kipindi kilichosalia cha mashindano ya CHAN 2024.
Pia, katika kikao hicho Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limepatikana na makosa kadhaa ya kiusalama wakati wa mechi dhidi ya Morocco iliyofanyika katika Uwanja wa Moi – Kasarani.
CAF ilisema Kenya ilishindwa kutimiza masharti ya usalama na hivyo kutozwa faini ya Dola 50,000 (takriban Sh milioni 127 ).CAF imeonya kuwa endapo hali hiyo itaendelea mechi za timu ya taifa ya Kenya zinaweza kuhamishiwa katika uwanja mbadala.
Kenya imetakiwa kuongeza idadi ya askari kwenye eneo la uwanja na kuhakikisha barabara zinazouzunguka zinafungwa ipasavyo siku za mechi.
Vile vile, Shirikisho la Soka la Zambia (FAZ) lilipatikana na hatia ya kukiuka kanuni za vyombo vya habari wakati wa mkutano na waandishi wa habari kabla ya mechi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Zambia ilishindwa kumpeleka kocha mkuu kwenye mkutano wa lazima na waandishi wa habari. Kufuatia kosa hilo imetozwa faini ya dola za kimarekani 5,000 , zaidi ya shilingi milioni 12
The post CHAN 2024: Morocco, Zambia zapigwa faini, Kenya onyo first appeared on SpotiLEO.