LONDON: MABINGWA wa Europa League Tottenham Hotspurs wamemtangaza beki wao wa kati Cristian Romero kama nahodha mpya wa klabu hiyo baada ya kuondoka kwa ‘Legend’ wa klabu hiyo Son Heung-min aliyetimkia ligi kuu ya Marekani MLS.
Son, ambaye alivaa kitambaa hicho cha unahodha kwa misimu miwili iliyopita na kunyanyua taji la Europa mwezi Mei wakimaliza ukame wa mataji wa miaka 17 alijiunga na Los Angeles FC ya Marekani mapema mwezi huu.
Romero alikuwa nahodha msaidizi kwa misimu miwili iliyopita na alianza katika kikosi kilichoibomoa Manchester United kwenye mchezo wa fainali wa Europa League kama nahodha kabla ya Son kuingia akitokea benchi kipindi cha pili.
Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 27 ataiongoza timu yake watakapovaana na mabingwa wa UEFA Paris Saint-Germain katika mchezo wa UEFA Super Cup usiku wa leo Jumatano.
“Nilikuwa na mazungumzo mazuri na Cuti Romero na atakuwa nahodha wetu mpya amejisikia kuheshimiwa sana na kufurahishwa sana na hatua hii. Ni jambo kubwa na sasa anapaswa kuwa kongozi wa klabu uwanjani, sio tu kwa Kombe hili la Super Cup, lakini pia msimu mzima. ” – Meneja mpya wa Tottenham Thomas Frank aliambia tovuti rasmi ya klabu.
Romero ambaye alijiunga na Spurs kutoka Atalanta miaka minne iliyopita alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Argentina ambacho kilishinda Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.
The post Spurs yampa Romero viatu vya Son first appeared on SpotiLEO.