……..
Wizara ya Nishati imedhamiria kuhakikisha Watanzania wote wanatumia nishati safi ya kupikia kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yameendelea kusababisha madhara makubwa kwa afya za wananchi na mazingira.
Serikali imesisitiza kuwa imeweka mkakati thabiti kufikia malengo haya, huku ikiwapongeza wadau wa maendeleo kama Oryx Gas kwa kushiriki kikamilifu katika juhudi hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni maalum ya Gesi Yente kwa kushirikiana na Oryx Gas, Mkurugenzi Mkuu wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay, alieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuhamasisha Watanzania kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.
“Kutotumia nishati safi kuna madhara makubwa ya kiafya na kimazingira. Tunaona jinsi miti inavyokatwa kwa wingi ili kupata kuni na mkaa. Hali hii inapaswa kubadilika,” alisema Mlay.
Aliongeza kuwa Serikali imepanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, takriban asilimia 84 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mlay alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau kama Oryx Gas ni muhimu kufanikisha dhamira hiyo.
“ORYX GAS wamekuwa msaada mkubwa. Wapo kila kona ya Tanzania na wameonyesha dhamira ya kushiriki kikamilifu kufanikisha mpango huu wa kitaifa,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mlay, Serikali pia iko kwenye mchakato wa kupunguza kodi katika bidhaa za nishati safi ili kufanya bei kuwa nafuu kwa kila Mtanzania.
“Tunatambua kuwa kodi kubwa husababisha bidhaa kuwa ghali. Tayari tumeandaa rasimu ya mapendekezo ya kushusha kodi ili wananchi waweze kumudu gharama za gesi ya kupikia,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania, Araman Benoit, alisema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha matumizi ya nishati safi kupitia kampeni mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Gesi Yente.
“Tunaishi katika kipindi ambacho afya ya jamii na mazingira vinahitaji ulinzi wa hali ya juu. Bado kuna familia nyingi zinazotegemea kuni, mkaa na mafuta ya taa kwa kupikia – hali inayochangia magonjwa ya njia ya hewa, uharibifu wa mazingira, na gharama kubwa za maisha,” alisema Benoit.
Kupitia kampeni ya Gesi Yente, Oryx Gas inalenga kurejesha mitungi ya gesi iliyopakiwa na kusahaulika majumbani na kuirudisha kwenye matumizi salama na bora.
“Mitungi hii ni rasilimali muhimu. Inaweza kusaidia familia nyingi kupika kwa usalama, haraka, na kwa gharama nafuu,” alisisitiza.
Aidha, Benoit alitangaza kuwa Oryx Gas itatoa zawadi mbalimbali kwa washiriki wa kampeni hiyo, ikiwa ni pamoja na pikipiki, baiskeli, seti za sufuria, na mabegi ya shule, kama motisha ya kuhamasisha matumizi ya gesi.
“Huu ni wakati wa kuamka kama taifa na kumuunga mkono Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kulifikisha taifa kwenye viwango vipya vya matumizi ya nishati safi. Kama una mtungi wa gesi nyumbani ambao huutumii – rudisha sokoni, tumia tena, na ujishindie zawadi! Na kwa wale ambao bado hawajaanza kutumia gesi, huu ndio wakati wa kufanya uamuzi sahihi kwa afya yako, familia yako, na mazingira yetu.”