Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa,akisisitiza jambo kwa Waandishi wa Habari kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa (hayupo pichani) wakati akizungumzia kuhusu Maendeleo ya Sekta ya Afya nchini leo Agosti 15,2025 katika Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.
Ofisi za Kanda za Bohari ya Dawa (MSD) jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi nchini , hatua ambayo imeongeza uwezo wa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, idadi ya vituo vinavyohudumiwa na MSD imeongezeka kutoka 7,095 mwaka 2021/22 hadi kufikia 8,776 mwaka 2024/25,idadi hiyo sawa na ongezeko la vituo 1,681.
Msigwa ameeleza kuwa vituo hivyo vinahudumiwa kupitia kanda 10 za MSD zilizopo katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mwanza, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Kagera, Mbeya na Iringa.
Pia, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, serikali imetoa Sh. bilioni 196.3, kati ya bajeti ya Sh. bilioni 200, iliyokuwa imewekwa, sawa na asilimia 98, fedha hizi zimetumika kununua dawa na vifaa tiba.
Msigwa amesema, serikali imevunja rekodi kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya dawa na vifaa tiba, tangu kuanzishwa kwa MSD mwaka 1994.
“Tumeandika rekodi ya kutoa fedha nyingi za vifaa tiba na dawa kuliko wakati mwingine wowote. Tangu kuanzishwa kwa MSD, hatujawahi kufikisha asilimia 98 ya bajeti iliyowekwa,”amesema.
Ameongeza kuwa mfumo huo utakuwa chachu ya mageuzi makubwa katika udhibiti wa bidhaa za afya nchini kwa kuwa utaongeza uwazi, uwajibikaji na usalama kwa watumiaji wa dawa.
“Lengo letu ni kuhakikisha dawa zote zinazotolewa kupitia MSD ni bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa,” amesisitiza