DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars Leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam dhidi ya Central Afrika Republic (CAR) kusaka ushindi na historia ya kumaliza hatua ya makundi kwa kushinda michezo yote katika mashindano ya Mataifa ya Afrika (CHAN 2024).
Mechi hii inatofautiana malengo Tanzania inatafuta rekodi mpya, huku CAR ikijaribu kuondoka kwa heshima.
Kwa Tanzania, ushindi dhidi ya CAR utamaanisha rekodi ya kipekee ya kushinda mechi nne mfululizo katika historia ya mashindano haya.
Kocha Hemed Morocco ameeleza wazi kuwa kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi.
“Tunataka kushinda mechi hii ya mwisho na kuandika historia mpya. Hakuna shinikizo kwa wachezaji wetu; kila mmoja anajua jukumu lake na kila mtu ana hamu ya ushindi,” alisema.
Kipa Aishi Manula aliweka wazi fahari yake: “Tumefika hatua hii kwa mara ya kwanza kushinda mechi tatu mfululizo. Afrika sasa inajua Tanzania. Timu zetu za klabu na taifa zinaendelea kupanda kiwango, na tunatarajia kufanikisha matokeo makubwa katika mashindano haya,” alisema Manula.
Kwa upande wa CAR, kocha Sebastien Ngato amekiri changamoto zilizowakabili, lakini amesisitiza kuwa mechi ya mwisho siyo ya kuondoka kimya bali ya heshima.
“Tunataka kuondoka kwa heshima, angalau tukipata pointi moja. Tumejifunza mengi katika mashindano haya na tunataka kuonesha mapenzi yetu kwa soka,” alisema Ngato.
Kocha Ngato aliongeza kuwa, licha ya kushindwa mara tatu, kikosi chake kitaingia uwanjani bila woga, wakiwa na nguvu za kisaikolojia na umakini.
“Tanzania itakuwa chini ya shinikizo, sisi tutacheza kwa uhuru na kujaribu kuonesha uwezo wetu.”
The post Stars kusaka heshima na historia leo first appeared on SpotiLEO.