Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiry Mkalipa, akifungua Kongamano la Kitaifa la Hijja, kwa naba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,leo.
2.Pic 25-Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, akitoa salamu za BAKWATA, katika Kongamano la Kitaifa la Hijja, leo jijini humu.

Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar, Suweid Ali Suweid, akwasilisha mada ya umuhimu wa Hijja leo, katika Kongamano la Kitaifa jijini Mwanza.

Baadhi ya viongozi wa taasisi za kiislamu wakiwa katika Kongamano la Hijja, leo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Msikiti wa Ijumaa, Alhaji Abdallah Amin Abdallah (katikati aliyevaa koti), akifutilia mada katika kongamano hilo.

Baadhi ya aknanamama wa Kiislamu wakiwa katika Kongamano la Kitaifa la Hijja, leo.

Baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Wanawakw wa Kiislamu Tanzana (JUWAKITA), Mkoa wa Mwanza, waliohudhura Kongamano la Ktafa la Hijja, leo. Picha zote na Baltazar Mashaka
………….
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Serikali mkoani Mwanza imelitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Mwanza, kuendeleza ushirikiano na taasisi zake kuratibu safari za mahujaji wanaokwenda kuhiji mwaka huu wa 1447 Hijria, huku ikiahidi kusaidia Waislamu kuhakikisha wanatimiza nguzo hiyo muhimu ya dini yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiry Mkalipa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, leo, wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Hijja lililofanyika jijini Mwanza.
Akizungumza mbele ya mamia ya waumini na viongozi wa dini Kiislamu, Mkalipa alisema Serikali ipo tayari kushirikiana kwa karibu na BAKWATA kuhakikisha waumini wa dini hiyo wanapata fursa ya kuhiji Makkah mwaka huu.
“Tupo bega kwa bega na taasisi za dini. Tutaratibu safari ya Hijja, tutafahamu idadi ya wanaokwenda na kuunga mkono mahitaji yao ili waweze kushiriki ibada hii tukufu,” amesema Mkalipa.
Pia , serikali katika kongamano hilo, imetoa rai kwa waislamu kuwekeza katika elimu ya watoto wao ikiwemo elimu ya dini, ili kuimarisha msingi wa imani na kumfahamu Mwenyezi Mungu katika hatua za awali za maisha.
“Kama tunataka kizazi kinachomcha Mungu, hatuna budi kuwekeza katika elimu bora. Tuwaandae watoto wetu waifahamu misingi ya dini, waepuke njia za mkato na uongo unaoharibu jamii,” amesisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
Mkalipa amewahimiza masheikh kuandaa semina kila mara kwa ajili ya wanaojiandaa kuhiji pia, watumie jukwaa hilo kuwaelimisha vijana tofauti ya uchumi halali na haramu, huku akisisitiza umuhimu wa kutenga muda wa kuelezea masuala ya zaka katika makongamano kama hayo.
“Masheikh, vijana wetu wanaotafuta uchumi wanahitaji maarifa ya kiuchumi kwa mujibu wa dini. Msiwaache waendelee kwenye biashara zisizo halali kwa kukosa uelewa. Elimisheni, fundisheni misingi ya halali na haramu,” amesema.
Aidha, amewahimiza viongozi wa dini kuwekeza katika ardhi kwa maendeleo ya Waislamu; “Ardhi ya bei nafuu inaisha. Nunueni kwa wakati huu na kuiweka chini ya BAKWATA kwa ajili ya vizazi vijavyo.”
Naye Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar, Sheikh Suweid Ali Suweid, katika kongamano hilo ameeleza kuwa, Hijja ni wajibu wa kila Muislamu mwenye uwezo, kuna umuhimu wa kuwasaidia wasio na uwezo ili watimize ibada hiyo.
“Tushirikiane kwa mambo ya kheri.Tukatae dhana ya kuwa sisi ni masikini wa milele. Mwanza ina watu zaidi ya milioni 3. Ni wakati sasa watu 400,000 waruke kwa ndege kwenda kuhiji,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Sheikh Othman Hamis Juma aliwasilisha mada kuhusu “Dhana ya Uwezo wa Kwenda Hijja”, akifafanua kuwa kila mtu ana uwezo wa kuhiji endapo ataweka mipango sahihi na kumtegemea Mwenyezi Mungu.
“Mwenyezi Mungu ana neema nyingi zisizopimika. Lakini haziji bila utaratibu. Kutamani pekee hakutoshi, lazima kuwe na matumaini na maamuzi. Jisogezeni kwa Mungu kwa Sunna, atawapa uwezo,” amesema Sheikh Othman.
Akitoa salamu za BAKWATA, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, amesema kongamano hilo ni muhimu kwa elimu, kushirikishana maarifa, na kuhimiza mshikamano wa kidini miongoni mwa Waislamu.
“Hamjakosea kuleta kongamano hili Mwanza, ushiriki wa viongozi wa serikali ni ishara ya mshikamano unaojengwa baina ya dini na dola, kwa maendeleo ya kiroho na kijamii.
Mwaka huu wa 1447 Hijria, matarajio ni kuona idadi kubwa ya Waislamu wa Mwanza wakitimiza ibada ya Hijja, si tu kwa sababu ya uwezo wa kifedha, bali maandalizi, mipango na mshikamano wa dhati,” amesema.