NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAKILI Mwandamizi Ladslaus Komanya kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema wanaendelea kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria hasa yaliyopo katika Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) ambalo mambo yake mengi yanayohusu utalaamu wa kisheria ikiwemo mikataba ya Kimataifa.
Ameyasema hayo leo Agosti 18,2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na TPDC ambayo yamewahusisha wadau kutoka sekta ya gesi na petroli pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Tumepata fursa kukutana na wenzetu wa TPDC kwa lengo la kupata mafunzo, kuhusu masuala mbalimbali yanayopatikana katika sekta ya gesi na petroli.TPDC ni taasisi hapa nchini inayofanya usimamizi na kimsingi sisi kama ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali tumekutana na wenzetu wa TPDC wametupitishe katika maeneo wanayofanyia kazi katika sekta hii.
“Kwa maana ya kujua sheria mbalimbali lakini pamoja na kujua namna wanavyofanya uwekezaji katika sekta hii na pia kufahamu kufahamu faida zinazopatikana katika sekta hiyo ya petroli na gesi.Pia kuona muelekeo na sisi kama ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali kuona mwelekeo wa Dira 2050.”
Pamoja na mambo mengine amesema sekta hiyo inahusisha masuala mengi ya kisheria hususani kuhusu mikataba, kufanya upekuzi wa mikataba, kwa sababu taasisi hiyo kwa asilia ya majukumu yake inafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kimataifa.
“Kwasababu sekta hii ni nyeti, utaona utalaamu unaweza usiwe kwa kiasi kikubwa hivyo unategemea zaidi wataalamu kutoka nje hivyo tunaingia mikataba mbalimbali na ni vizuri sisi kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tunaipitia mikataba na kuipendekeza ile mikataba kabla haijasainiwa.
“Kwahiyo tuna kila sababu ya kujua yale yanayofanyika kiundani nje ya vitabu vya sheria kwa kufanya tafiti ,ni lazima tusikie kutoka kwenye taasisi yao ili tuweze kufanya kazi zao kwa usahihi.
“Hatufanyi mafunzo haya sisi wenyewe ofisi ya mwanasheria mkuu bali pia tunatarajia kusikia kutoka kwenye taasisi nyingine kama PPRA, PURA pamoja na wenzetu wa sekta ya petroli na gesi kutoka Zanzibar ambao nao wanashiriki mafunzo.”
Aidha amesema wanatarajia kujifunza mambo mengi ili watakaporudi maofisini kwao wafanye shughuli zao kwa ubora na weledi zaidi.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka TPDC, Elias Mwashiuya amesema mafunzo hayo ni sehemu ya kujengeana uwezo kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara katika sekta ya nishati.
“Kuna timu mpya zinazoundwa ndani ya serikali, wengi wanaingia bila uzoefu wa moja kwa moja wa namna ya kushughulika na sekta hii. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na matukio kama haya mara kwa mara ili kujifunza, kukumbushana na kujenga uwezo wa pamoja,” alisema Mwashiuya.
Aidha, Mwashiuya alibainisha kuwa mafunzo hayo yataendelea kufanyika mara kwa mara kwa ushirikiano kati ya TPDC na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.